Rebecca Butcher; ni mrembo mwenye umri wa miaka 24 kutoka katika Kitongoji cha Barnsley, South Yorkshire nchini Uingereza ambaye ameibuka kueleza kuwa wakati anavunja ungo alipokuwa na miaka 13 au 14 alijigundua titi moja pekee ndilo linakua kifuani mwake huku lingine la upande wa kushoto likiwa haliongezeki au kukua.
Rebecca anasema kuwa, alikwenda hospitali ila daktari akamwambia kwamba titi lingine litachomoza na kukua baada ya muda, lakini hakuna kilichotokea hadi sasa licha ya kurudi kwa madaktari mara kadhaa pia mpaka sasa hajafanyiwa uchunguzi rasmi na kuambiwa tatizo ni nini hasa.
Rebecca anadai kuwa, hata baadhi ya madaktari aliowafuata pia hawajui imesababishwa na nini.
Anasema kuwa, hali ya kuota titi moja pekee ilimsababisha aanze kujisikia aibu hivyo upande mmoja wa kifua chake akawa anajaza soksi na kuvaa sidiria na nguo zinazofika shingoni ili kuficha hali yake.
Anaongeza kuwa, baada ya kuona madaktari hawampi jibu la kueleweka, alijaribu kufanya utafiti mwenyewe, akagundua kuna tatizo linaloitwa Poland Syndrome kama linahusiana na hilo lake ila hana uhakika wa moja kwa moja kwa sababu madaktari wengine walimuambia hawajui tatizo ni nini.
Hata hivyo, kwa sasa amesema ameamua kuikubali hali yake hiyo aliyozaliwa nayo maisha yanaendelea.