Vijana wa sasa wana bahati ya mtende kwa sababu wamebarikiwa fursa ya teknolojia, lakini kuwa na teknolojia tu haitoshi, mchawi mwenzake ni UBUNIFU!
Sasa sikia; mwamba mmoja ambaye ni kinyozi nchini Nigeria ameongeza ubunifu kwenye kazi yake hiyo baada ya kuwa anawanyoa wateja wake kwa kutumia vifaa vya kufanyia hisabati (compass) kisha kurekodi video na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii ili kuvutia wateja ambao sasa wanamiminika kwenye saluni yake.
Katika moja ya video za jamaa huyo anaonekana akitumia vifaa vya hisabati vya kuchora kama rula, pembetatu, mduara, bikari na dira ambapo anapima kwanza kichwa na kuweka alama muhimu kama nyuzi 90, nyuzi 45, mduara, pembetatu, mastatili, mraba na nyinginezo kabla ya kumnyoa.
Watu wengi wamekuwa na maswali wakishangaa kama kinyozi huyo alikuwa mwalimu wa hisabati awali au pengine kazi ya ualimu ilimpiga chenga akaamua afungue kinyozi!
Hata hivyo, kwa mujibu wa maoni ya wengi, ni kwamba wanatamani mno kunyolewa kwa ufundi kama huo na wengine wenye biashara kama hiyo kutaka kujifunza ufundi huo wa kipekee.