Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MUSIC FACTS: Soggy alimpata DK Remmy kwa mzinga wa Konyagi!

Soggypic Soggy Doggy

Mon, 2 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Alianza muziki shuleni katika kundi la Bantu Pound Gangsters, tofauti na wengi wanavyodhani Soggy Doggy hajawahi kushawishika na muziki wa rapa wa Marekani, Snoop Doggy, bali kiu yake ya kufanya muziki ilipopamba moto baada ya dada yake kumnunulia albamu ya Saleh Jabir.

Huyu pia ni prodyuza ambaye ameshiriki kuanza kazi nyingi kubwa ndani ya Bongo Records ila awali Soggy alishafanya kazi FM Studios. Bongo Music Facts inakuja zaidi;

1. Jina la Soggy Doggy asili yake ni kipindi akiwa mdogo alikuwa anapenda sana kukaa kwenye maji, ndipo akajiita ‘Soggy’ hilo ‘Doggy’ lilikuja alipoenda kusoma Mbeya kuna mwalimu aliwaita ‘mbwa” ndipo wanafunzi wakaanza kujiita dog, na kisha likazaliwa jina la Soggy Doggy.

2. Hayati Misanya Bingi ndiye alimlipia Soggy fedha ya kurekodi wimbo wake wa kwanza katika studio kubwa, MJ Records ambapo kurekodi ilikuwa ni Sh10,000 hiyo ni baada ya kutumbuiza kwenye beach party aliyokuwa anasimamia DJ Boniluv.

3. Ilimbidi Soggy Doggy kumnunulia mizinga miwili ya Konyagi, Remmy Ongala ili aweze kushiriki kwenye albamu yake ya kwanza ‘Bongo New York’, watu wa bendi ya Remmy, Orchestre Super Matimila ndio walimshauri Soggy kufanya hivyo wakati huo alikuwa bado ni mwanafunzi.

4. Soggy na Bizman ndio wametengeneza mdundo wa wimbo wa Bushoke ‘Mume Bwege’ na kurekodi ndani ya Bongo Records siku hiyo P Funk Majani hakuwepo studio, aliporudia akakuta kila kitu kimekamilika, yeye akamalizia upande wa mixing na mastering.

5. Ndani ya Bongo Records, Soggy Doggy ameshiriki kutengeneza ngoma za Ngwea kama She Got A Gwan na Mikasi ambapo alishirikiana na Mzungu Kichaa na Profesa Ludigo pia ndiye alirekodi ‘vocal’ za wimbo wa Ngwea, Sikiliza.

6. Wakati wimbo wake, Kibanda cha Simu unafanya vizuri bado Soggy alikuwa analipwa kati ya Sh100,000 hadi Sh150,000 kwa shoo moja. Mwaka 2013 ndipo Soggy alipata shoo aliyolipwa fedha nyingi zaidi ikiwa ni Sh1.5 milioni mkoani Mwanza.

7. Katika maisha yake ya muziki Soggy ametoa albamu tano, wasanii waliomzidi kwa idadi ya albamu ni Sugu mwenye albamu zaidi ya 10, Lady Daydee mwenye albamu nane. Jide anaongoza upande wa wasanii wa kike ndani ya Bongofleva.

8. Soggy ndiye mtu wa kwanza kumpa Salama Jabir nafasi ya kutangaza redioni, wakati huo Soggy alikuwa anafanya kazi Times FM ndipo Salama akaanza kazi ya redio na alikuwa akitangaza kipindi cha jioni.

9. Soggy Doggy ana mchango mkubwa kutoka kimuziki kwa Dogo Hamidu ambaye sasa anajulikana kama Nyandu Tozzy. Soggy ndiye alimuingiza kwenye kundi la Hotpot Family na baadaye akaenda Dar Skendo kwa Dudu Baya.

10. Mwana FA ndiye alimtafutia gari la kwanza alilonunua Soggy, hiyo ni baada ya kupokea malipo ya albamu yake kiasi cha Sh6 milioni ambazo aligawana nusu kwa nusu na P Funk Majani aliyekuwa anasimamia kazi zake.

Soggy akachukua takribani Sh3 milioni na kumkabidhi Mwana FA ambaye alitafuta gari hilo. Chid Benzi ndiye alikuwa shahidi wa Soggy wakati anasaini makubaliano ya kununua gari hilo. Na fedha alizopata kwenye mauzo ya albamu yake ya kwanza ndizo alizotumia kulipa ada ya chuo.

Chanzo: Mwanaspoti