Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MUSIC FACTS: Maegesho ya magari ndio yamemtoa Rayvanny kimuziki

RAYVANNY FIESTA Maegesho ya magari ndio yamemtoa Rayvanny kimuziki

Tue, 10 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Alianza kama msanii wa Rap kama ilivyokuwa kwa Aika wa Navy Kenzo, Lady Jaydee, Diamond Platunumz, Dayna Nyange na wengineo, baadaye akageukia uimbaji hadi kuivutia WCB Wasafi iliyomsaini na kumtoa kimuziki.

Huyu ni rais wa lebo ya Next Level Music (NLM), ametoa albamu moja, Sound From Africa (2021) na EP tu; Flowers (2020), New Chui (2022) na Flowers II (2022), huku akishinda tuzo kubwa duniani. Bongo Music Facts inakujuza zaidi;

01

Ni msanii wa kwanza toka Afrika kutumbuiza katika hafla ya utoaji wa tuzo za MTV Europe Music Awards (MTV EMA) 2021 nchini Hungary, akitumbuiza wimbo wake 'Mama Tetema' alioshirikiana na Maluma kutokea Colombia, wimbo huu ulishika nafasi ya kwanza chati za Billboard Mexico Airplay.

UPO MWENYEWE

Ndio jina la wimbo wake wa kwanza kuurekodi na kuuachia akiwa chini ya Tip Top Connection aliyojiunga nayo mwaka 2012, haukufanya vizuri kutokana wakati anautoa hakuwa kwenye maelewano mazuri na Babu Tale ambaye ndiye aliyemleta kwenye kundi hilo.

02

Ni msanii wa pili Afrika Mashariki na wa kwanza Tanzania kushinda tuzo ya BET (2017), Staa wa Uganda, Eddy Kenzo ndiye binadamu wa kwanza ukanda huo kushinda tuzo hizo zinazoandaliwa na Black Entertainment Television (BET) Marekani tangu Juni 19, 2001 kwa lengo la kusheherekea mafanikio ya kazi za Wamarekani Weusi katika sanaa ya muziki, uigizaji na michezo.

MBOSSO

Ndiye aliyempigia simu Rayvanny na kumwambia aende studio ndipo alipokutana na Diamond hadi kuona uwezo wake na kuja kumsaini WCB Wasafi, kipindi hiki Rayvanny alikuwa anafanya mazoezi kituo cha Mkubwa na Wanae na kuzunguka kwenye show za kundi la Yamoto Band alilokuwepo Mbosso.

03

Idadi ya nyimbo za wasanii wakubwa zinazotambulika ambazo Rayvanny alishiriki katika uandishi na kuchangia melodi, nyimbo hizo ni 'Zigo Remix' yake AY akimshirikisha Diamond Platnumz, 'My Life' yake Dogo Janja na 'Make Me Sing' ya Diamond akimpa shavu AKA wa Afrika Kusini.

FAHYMA

Ndiye mrembo ambaye ameonekana kwenye video nyingi zaidi za Rayvanny, Fahyma ametokea video za nyimbo kama; Kwetu, Natafuta Kiki na Siri. Na ikumbukwe Mwanamitindo huyo aliyeshinda tuzo kama Scream (Nigeria) na Starqt (Afrika Kusini) ndiye mzazi mwenziye Rayvanny wakiwa wamejaliwa mtoto mmoja.

08

Idadi ya nyimbo ambazo Rayvanny ameshirikiana na Diamond Platnumz na ndio wasanii waliofanya kolabo nyingi zaidi Bongo kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita. Nyimbo hizo ni kama Salome, Iyena, Mwanza, Tetema, Timua Vumbi, Amaboko, Woza na Nitongoze uliotoka baada ya Ravanny kuondoka WCB Wasafi.

RAV4

Gari lake la kwanza kukabidhiwa na WCB Wasafi, lebo aliyofanya nayo kazi kwa miaka saba na kupata mafanikio makubwa hadi kuja kuanzisha yake, NLM hapo Aprili 2021 na kumsaini Mac Voice ambaye mwaka huo alichaguliwa kuwania tuzo za AEAUSA kama Msanii Bora Chipukizi lakini hakushinda kama ilivyokuwa kwa Rayvanny mwaka 2016.

2016

Mwaka alioachia wimbo wake wa kwanza 'Kwetu' uliomtoa kimuziki, wazo la kuandika ngoma hii lilimjia akiwa ameketi eneo la maegesho ya magari baada ya kuzuia kuingia kwenye mahojiano katika kituo kimoja cha redio baada ya kukosa kitambulisho maana jina lake halikuwekwa kwenye orodha ya wageni.

MILIONI 860

Ni msanii wa pili nchini Tanzania aliyetazamwa zaidi YouTube kwa muda wote akiwa na 'views' zaidi milioni 860.3 tangu ajiunge na mtandao huo Machi 17, 2016, ametanguliwa na Diamond Platnumz mwenye 'views' zaidi bilioni 2 na ndiye anaongoza katika nchini za kusini mwa Jangwa la Sahara.

Chanzo: Mwanaspoti