Msanii mkongwe ambaye pia ni kati ya waanzilishi wa Bongo Flava, Mr Nice amezungumza kwa kujitapa kwamba hakuna msanii katika kizazi cha sasa na hata kizazi kijacho ambaye anaweza kumpiku katika rekodi za mauzo ya muziki wake, na kiwango cha maokoto ambayo alipata kutokana na usambazaji wa kazi zake.
Mkali huyo wa ‘Fagilia’ alikuwa akizungumza kwenye mahojiano na kituo cha Clouds nchini Tanzania ambapo alijipiga kifua kwamba kipindi hicho majukwaa ya kidijitali ya kupakua, kutiririsha na kusambaza miziki hayakuwepo lakini alipiga kazi ya kiume kwenye kutengeneza hela ndefu, rekodi ambayo amesema haitokuja kuvunjwa hata katika karne moja ijayo.
Mr Nice alisema kuwa kipindi hicho alisambaza mikanda ya CD ipatayo Zaidi ya milioni moja na kujizolea maokoto ya Zaidi ya bilioni 10 pesa za Tanzania.
“Hakuna mtu anayeweza kufikia rekodi yangu. Kama kuna mtu ambaye anaweza kuifikia si aje hapa aseme. Lakini wanajua hawawezi. Mimi nilikuwa nauza CD, nilikuwa siuzi Online. Na kama niliweza kuuza Zaidi ya CD milioni moja; wachana na Tapes, wachana na VHS. Hizo ni CDs pekee. Nilitengeneza mamilioni, kitu ambacho hakuna msanii anaweza akatengeneza sasa hivi,” Mr Nice alisema.
Msanii huyo alikuwa kidogo anakasirika baada ya mtangazaji kumtaka ataje ni milioni ngapi aliweza kutengeneza kwa kukadiria.
Mr Nice alihisi kuchefuka roho akisema kuwa mtangazaji alikuwa anamkosea heshima akisema ni kiwango na mamilioni alitengeneza wakati yeye alipiga Zaidi ya kiwango cha mabilioni.
“Eti unauliza kama iliweza kufika bilioni moja? Kaka hebu niulize swali jingine.. mimi nilipiga Zaidi ya bilioni 10 kwenda mbele huko,” aliongeza.
Msanii huyo alisema kuwa wengi wanadhani wasanii wa kitambo akiwemo yeye na wengine kama TID Mnyama wanaishi maisha ya ukabwela sasa hivi bila kujua michango yao mikubwa katika tasnia ya muziki miaka ya nyuma na jinsi iliwajenga pakubwa kiasi kwamba hawatokuja kukaa wakaanza kutembeza sahani barabarani wakiomba msaada.