Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MC ajenga ukumbi wa bilioni 1.5, vijana wapewa ujumbe

MC Ajenga Ukumbi .jpeg MC ajenga ukumbi wa bilioni 1.5, vijana wapewa ujumbe

Mon, 4 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mchungaji wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) jijini Dodoma, Wisdom Gowele ametoa wito kwa vijana kutumia nguvu zao ujanani kuwekeza katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo badala ya kuendekeza starehe na uzeeni kuishia kuwa ombaomba.

Mchungaji huyo wa Ilazo, ametoa wito huo jana Alhamisi jijini Dodoma katika ibada maalumu ya kuweka wakfu ukumbi wa mikutano uliojengwa na mshereheshaji maarufu jijini hapa, Mc John Mwangata  kwa gharama ya zaidi ya Sh 1.5 bilioni.

Ukumbi huo wenye uwezo wa kubeba watu zaidi ya 600 umejengwa katika eneo la Maungu karibu na Mnada mpya wa Nkuhungu barabara ya Singida kilometa tisa kutoka mjini Dodoma.



Mchungaji Gowele amesema vijana wengi wamekuwa wakipambana kutafuta hela lakini wengi hujikita zaidi katika masuala ya anasa badala ya kuwekeza katika masuala ya kimaendeleo.

“Vijana mnatakiwa kujua kuwa kazi zinakuja na kuisha, ujana pia ni maji ya moto na kuna wakati wa kufanya kazi ukiwa na nguvu hivyo vijana nataka kuwaambia kuwa mnatakiwa kuwekeza miradi mikubwa mkiwa na nguvu.

“Fanyeni uwekezaji hususani kwa kutumia fursa zilizopo katika makao makuu ya nchi na mkiwekeza mtasaidia kuongeza pato la taifa, mtu binafsi pamoja na jamii kwa ujumla wake jambo ambalo litawafanya waliowengi kuondokana kukaa vijiweni” ameeleza Mchungaji Gowele.

Kwa upande wake Mwekzaji wa Ukumbi wa mikutano wa Mwangata social Hall, Mc John Mwangata aliwasihi wasanii pamoja na washereheshaji wenzie nchini kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kula ‘bata’ badala yake wafanye shughuli zao kwa kuamini kuwa wanachokifanya ni sehemu ya ajira yao.

Amesema ameamua kufanya uwekezaji huo ikiwa ni sehemu ya kuweka alama ya kazi yake ya ushereheshaji.

“Kazi ya ushereheshaji ni kazi yenye kipato kidogo lakini ukijipanga unaweza kufanya kitu cha maana nimeamua kuwekeza katika ukumbi wa mikutano na shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuwa iwapo nitakuwa nimeachana na shughuli hiyo nitakuwa na sehemu ya kujishikiza na kujipatia kipato.

“Najua kuwa uwekezaji huu ni mkubwa kwani mpaka nakamilisha nimetumia zaidi ya Sh. 1.5 bilioni na una uwezo wa kuchukua watu 600 kwa wakati mmoja jambo ambalo naweza kujivunia katika kazi zangu za ushereheshaji ndani ya miaka 20” amesema Mc Mwangata.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live