Mchekeshaji aliyeokoka MC Willy Grayson amesema kuwa hakuwahi kujua kama mkewe ni mtoto wa mwimbaji maarufu wa muziki wa Injili, Christina Shusho.
Akihojiwa na chombo kimoja cha habari hapa nchini, MC Willy amesema; "Mke wangu kabla sijamuoa nilikuwa namuona tu kanisani na wala hatufahamiani. Nikamuona Instagram siku moja na alikuwa ameposti wimbo wake, nikauchukua nikauposti insta story yangu ndipo akanitumia ujumbe kushukuru.
"Toka hapo tukawa marafiki akiona nimeposti ana-comment na nilikuwa namuita dogo, nilipoona vitu ninavyovipenda kwake ndipo tukaamua kuingia kwenye mahusiano na mpaka nimemuoa.
"Nilipoanza mahusiano na mke wangu nilikuwa namwambia tu kuwa jina lako linafanana na Christina Shusho na akawa ananiambia tu labda ni ndugu yangu na kulikuwa na wigi lake akivaa namwambia ukivaa hili wigi unafanana na Christina Shusho anacheka.
"Mke wangu alikuwa mnyenyekevu sana. Anapanda daladala, tunakula chipsi za vibandani na akikuta chipsi yai 3000 anakataa anasema twende kwenye chipsi za 2500. Ukimuangalia hajulishi hata kama kwao kuna gari. Baadae sana ndio aliamua kufunguka mwenyewe kuniambia yeye ni mtoto wa Shusho wakati huo tayari tuko kwenye mahusiano na umeshapita muda mrefu sana," amesema MC Willy.