Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MASTORI YA OSCAR: Marioo unamkumbuka dogo Aslay enzi hizoo?

Marioo Pic Marioo unamkumbuka dogo Aslay enzi hizoo?

Mon, 18 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Hakuna ubishi kwenye gemu ya Bongofleva kama Marioo. Huwezi kwenda klabu yoyote ile nchini usisikie nyimbo zake kila baada ya nusu saa. Ni msanii anayekubalika sana kwa sasa. Ni msanii mwenye hit song nyingi sana kwa sasa. Nyimbo zake zote zinaimbika na kuchezeka na kila mtu. Tanzania tuna tatizo kubwa la kutengeneza mastaa wengi wa tasnia moja kwa muda mrefu. Tuliwahi kuwa na Hasheem Thabeet kwenye kikapu mpaka ameondoka kama nchi hatujawahi kupata mtu wa aina ile.

Tumekuwa na Mbwana Samatta kwenye soka mpaka ataondoka, huoni mtu mwingine wa kiwango kile. Tumekuwa na Diamond Platinumz kwenye muziki, lakini mpaka sasa huoni mtu mwingine anayekaribia walau mbio zake. Walau mafanikio yake. Nadhani kuna hatua moja wasanii wetu wengi wameshindwa kufika.

Nadhani kuna batani moja wameshindwa kuifikia. Namtazama Marioo kama msanii bora wa kizazi hiki cha Bongofleva, lakini bado naye anashindwa kwenda mbele zaidi.

Baada ya kuteka soko la Bongo, bado sizioni harakati zake za kuteka soko la Nigeria. Bado simuoni Marioo akiteka soka la Kenya, Uganda na Rwanda kama alivyofanya Diamond. Sina tatizo na uwezo wake hata kidogo. Ni msanii wa kiwango kizuri na yuko kwenye wakati wake. Hapa ndiyo mahali ambapo wasanii wengi huishia na baadaye kuanza kurudi nyuma.

Muziki ni kama zilivyo tasnia nyingine. Ni suala la zama ukishindwa kutumia vyema time yako, mtu mwingine ataibuka. Aslay ni moja kati ya wasanii waliowahi kuwa juu kwenye Bongofleva kama alivyo Marioo wa leo. Aslay alikuwa anakwenda kwenye shoo na watu wanaimba nyimbo zake mwanzo mwisho. Aslay alikuwa ni msanii ambaye kila kona ya starehe nyimbo zake zilikuwa zinapigwa. Muda ulikuja, ukaisha, ukaondoka. Kuna muda kwenye soko la ndani alishamsogelea kabisa Diamond, lakini nje ya mipaka hakwenda mbali. Nadhani kuna batani hakuifikia. Nadhani kuna mstari wa kimataifa alishindwa kuuvuka. Kuna mahali Marioo anapaswa kuvuka kwa sababu huu ndio wakati wake. Hakuna ubishi kwa soko la ndani ameshinda kila kitu. Kwa soko la ndani watu wanapenda nyimbo zake. Tunahitaji kuwa na kina Diamond wengi tu nchini.

Tusipambane kumshusha Diamond ili kumpandisha mwingine. Huu ni wakati wa kuwatengeneza kina Diamond wengine. Hata kama tutakuwa na wasanii 10 wa kiwango cha Diamond, sio dhambi. Hapa alipofika Marioo kuna muda hata Barnaba Classic aliwahi kufika, lakini hakuvuka mstari. Hakwenda zaidi nje ya nchi. Soko lake lilibaki kuwa ndani tu na baadaye likapungua ubora.

Moja kati ya maeneo ambayo yanachangia ukuaji wa Diamond ni ushawishi wake kwenye mitandao ya kijamii. Diamond ana kurasa zenye wafuasi zaidi ya milioni 10 mtandaoni. Kuanzia mama, dada, mjomba wake (mume wa mama yake) na wasanii wake. Hao wakimposti tu mara moja mtandao unachafuka.

Diamond anajuana na watu wengi sana Tanzania. Mtandao huu hauji kwa bahati mbaya. Ni matunda ya juhudi zake. Marioo anahitaji kupata timu ya kumvusha na hasa kwenye soko la nje ya Tanzania. Lazima apate watu sahihi na mtaji wa kuweza kumvusha. Itapendeza kumuona naye akifika pale Diamond alipo ingawa haiwezi kuwa rahisi.

Vijana wengi wanaofanya Bongofleva kwa sasa, Diamond anafaa kuwa ‘role model’ wao. Vijana wengi wanaocheza kikapu Tanzania, Hasheem Thabeet anapaswa kuwa ‘role model’ wao. Wale wanaocheza soka, Samatta bila shaka yoyote anatosha kuwaonyesha njia. Unapotaka kwenda kimataifa ni lazima uwe na watu wenye welekeo huo. Lazima uwe na timu ya watu wanaojua mahitaji ya soko la kimataifa. Kwa kutazama tu uwezo Marioo ameshafika eneo la tukio. Lakini kama asipopata watu wa ukweli baada ya miaka mitatu, taratibu anaweza kuanza kurudi nyuma.

Marioo huu ndio muda wako wa kuiteka Afrika na dunia. Ni muda wa kufanya kazi kimataifa zaidi. Muziki ni tasnia ya wakati. Kuna muda wako na muda wa wengine. Kwa namna nchi nzima inavyoimba nyimbo zako, ni wakati wa kutengeneza timu kubwa ya kukusimamia. Muziki wa Marioo unapaswa kuimbwa kwa sasa na dunia nzima.

Leo ni Sikukuu ya Pasaka bila shaka yoyote kila kona ya nchi nyimbo za Marioo zinakwenda kutikisha. Itapendeza zaidi kama Pasaka ijayo, dunia nzima itakuwa inaburudishwa na kijana huyu wa Kitanzania a.k.a Mzee wa Bia Tamu!

Unadhani Marioo anapaswa kufanya jambo gani kutoboa kimataifa?

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz