Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lulu kuwa raia huru baada ya siku 39

20723 Pic+lulu TanzaniaWeb

Thu, 4 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Zimebaki siku 39 kati ya 484 ambazo mwigizaji Elizabeth Michael, maarufu Lulu anapaswa kutumikia jela.

Novemba mwaka jana, Lulu alipatikana na hatia ya kumuua bila kukusudia aliyekuwa mpenzi wake Steven Kanumba.

Msanii huyo ambaye sasa anamalizia kifungo chake akiwa mfungwa wa nje, alikaa gerezani kwa siku 184 kabla ya kubadilishiwa Mei 14 na kuwa mfungwa wa nje.

Kifo cha Kanumba ambaye pia alikuwa mwigizaji maarufu kilichotokea Aprili 7, 2012 kilimwingiza matatani binti huyo akiwa na umri wa miaka 17.

Lulu alitarajiwa kumaliza adhabu yake Machi 12, mwakani. Hata hivyo, katika maadhimisho ya Siku ya Muungano Aprili 26, Rais John Magufuli alitoa msamaha wa kupunguza robo ya adhabu kwa baadhi ya wafungwa, naye akawa miongoni mwa wanufaika.

Msamaha huo ulimpunguzia adhabu na sasa anatarajiwa kuwa huru kuanzia Novemba 12.

Katika kutumikia adhabu hiyo, Lulu amepangiwa kazi ya kufanya usafi katika Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iliyopo Posta Jijini Dar es Salaam aliyoianza tangu Machi 14.

Akizungumzia utendaji kazi wa Lulu, Mkuu wa Probesheni na Huduma za Jamii, Charles Nsanze, alisema katika kipindi chote hicho amekuwa akitekeleza majukumu yake bila kukosa.

“Amekuwa mmoja wa wafungwa wenye nidhamu ya hali ya juu na hakuna siku aliyokosa kuja na kufanya kazi kama alivyopangiwa,” alisema Nsanze.

Lulu amewahi kuigiza katika michezo ya Zizimo, Dira, Tufani, Taswira, Demokrasia na filamu za Family Tears, Oxygen, Women of Principle na Foolish Age.

Chanzo: mwananchi.co.tz