Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lulu amaliza kifungo, atokea mlango wa nyuma kukwepa waandishi

26700 Pic+lulu TanzaniaWeb

Tue, 13 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hatimaye msanii wa filamu, Elizabeth Michael maarufu kama 'Lulu', amemaliza kutumikia kifungo chake cha miaka miwili baada ya kupatikana hatia ya kuua bila kukusudia.

Akizungumza na waandishi wa habari, muda mfupi baada ya Lulu kumaliza taratibu za kifungo hicho leo Jumatatu Novemba 12, 2018 Mkurugenzi wa Idara ya Probesheni  Wizara ya Mambo ya Ndani huyo, Aloyce Musika, amesema Elizabeth Michael amemaliza salama na sasa ni mtu huru.

Lulu alikuwa akitumikia kifungo cha miaka miwili jela, baada ya Novemba 13, mwaka jana alipopatikana na hatia ya kumuua bila kukusudia aliyekuwa gwiji wa filamu nchini Tanzania, Steven Kanumba.

Tangu Mei 14 mwaka huu, Lulu alikuwa akitumikia kifungo hicho cha nje kwa kufanya kazi za usafi katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Ndani jijini Dar es Salaam.

Musika amesema katika kipindi chote Lulu amekuwa mtiifu kwa kila alichopangiwa na kama haitoshi walikuwa wakimfuatilia nyendo zake hadi anapoishi na ameonekana kuwa raia mwema na wameridhika kuwa amerekebishika.

Lulu awakwepa waandishi

Pamoja na baadhi ya waandishi wa habari kuweka kambi katika wizara hiyo kumsubiria Lulu kuwa anaweza kuongea chochote baada ya kuwa huru, jambo hilo liligonga mwamba baada ya kuondoka eneo hilo kwa ‘njia za panya’.

Mwandishi wa Mwananchi aliyepiga kambi wizarani hapo tangu saa 12.00 asubuhi alimwona Lulu ambaye alikuwa amevaa sketi iliyovuka magoti kidogo ya rangi ya kijani iliyoiva, na blauzi ya rangi ya maziwa yenye maua madogo madogo, wakati alipokuwa akielekea ofisi za waangalizi wake mara baada ya kumaliza kazi aliyokuwa amepangiwa kuifanya.

Mara baada ya kumalizia taratibu za kuachiwa huru, Lulu alionekana akirandaranda kwenye ofisi za maofisa waliokuwa wakimsimamia dalili zilizoonyesha wazi alikuwa akivizia namna ya kuwatoka waandishi waliokuwa wakimsubiria walau kupata hata picha yake kama si kuongea naye.

Pamoja na msimamizi wake Mwanaidi Makongoro kuwaeleza waandishi kuwa atakuwa huru kuongea kama atakubali mwenyewe baada ya kutoka ofisini kwao, ilionekana Lulu hakuwa tayari kwa hilo.

Ilipofika saa 4:45 mwandishi alimshuhudia Lulu ikiondoka kwa kupitia mlango wa nyuma wa ofisi za Idara hiyo zilizopo ghorofa ya nne.



Chanzo: mwananchi.co.tz