Aliyekuwa fotografa maalum wa CEO wa WCB, Diamond Platnumz, Ashraf Lukamba amesema kuwa hajaondoka katika Lebo hiyo kama baadhi ya watu wanavyosema, bali ameamua kufanya mambo yake mengine kwanza.
Lukamba ambaye alianza kufanya kazi na Diamond mwaka 2016, amesema baada ya kuhitimu masomo ya elimu ya msingi nyumbani kwao Kigoma, Uvinza alihamia Dar es Salaam kwa baba yake mzazi ambako alianza masomo ya kidato cha kwanza mpaka cha nne lakini hakupata matokeo mazuri ndipo akaamua kufanya biashara, baada ya mambo kuwa magumu alirejea darasani kujifunza masuala ya kupiga picha.
“Lavala ni mtu wa nyumbani sana, ni home boy tunajuana kitambo, kwa hiyo nilimshuti behind the scene ambazo baada ya kumwonyesha Diamond alizipenda akaniita ofisini, nilipofika akaniambia nianze kufanya kazi na Rayvanny, nikawa official fotografa wa kwanza wa Rayvanny.
“Alipokuja Rich Mavoko, kuna siku akawa anataka kusafiri kwenda Kenya na hakukuwa na mpiga picha, nikaondoka naye nilifanya kazi nzuri sana kule. Video zile alipoziona bosi Sallam SK akaniambia nitafute passport haraka. Baada ya hapo nikaanza kufanya kazi na Diamond na safari yangu ya kwanza nay eye tulienda kufanya kazi Afrika Kusini.
“Kwa sasa nimeamua kufanya kazi zangu nyingine, wala sio kwamba nina ugomvi na Diamond ama WCB, wale bado ni familia na Diamond tunawasiliana vizuri. Mara ya mwisho aliniambia alipoteza cheni yake Ureno.
“Siwezi kufuta utambulisho wa bio yangu kuwa mpiga picha wa Diamond, hiyo ni alama ipo tu haiwezi kufutika wala kubadili chochote. Ni historia iliyopo unaifutaje sasa?” amesema Lukamba.