Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

SIL

Lugha ya misimu ma mchango katika Kiswahili sanifu

815b85189999fe1cd1a7e8c2ab98f1f9.png Lugha ya misimu ma mchango katika Kiswahili sanifu

Sat, 28 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TUNAENDELEA na makala haya yaliyoanza wiki iliyopita kuhusu lugha ya misimu na mchango katika Kiswahili sanifu na leo tunaanza kwa kuangalia faida za misimu katika jamii.

Kwa watumiaji wa lugha wanaweza kujiuliza kwa nini maneno haya yanapewa nafasi katika matumizi ya lugha? Pamoja na ukweli kuwa maneno haya yaliyo mengi hutumika kwa kipindi fulani na kutoweka lakini misimu ina umuhimu kwa sababu ni maneno ambayo hutunza historia ya jamii ya watu hususani pale yanapoibukia.

Kwa mfano kuwapo kwake wakati fulani kama vile kwenye Vita vya Kagera kuliibuka maneno kama mtutu, nduli, joka ni baadhi ya maneno ambayo yalitumika sana.

Misimu pia husaidia kuiremba lugha ya jamii hii kwa kuwa mingi huibukia kwenye masihara na kejeli.

Kwa kuwa tumezungumza hapo awali kuwa misimu huanzia katika lugha zisizo rasmi kwenye lugha hii kuna ubunifu ambao unasababisha mawasiliano kuwa mafupi badala ya kuzungumza maneno mengi. Kwa mfano, neno utaipata ni neno la Kiswahili ambalo ukilizungumza tu kwa wale wajuzi wa lugha hiyo watakwambia kuwa neno hilo limefupisha maneno mengi ambayo yangezungumzwa kwa mtu ambaye unataka kumwambia kuwa atakuwa matatani katika jambo fulani.

Kwa kuwa tunasema kuwa misimu huibuka tu pale kunapokuwa na matukio kwenye jamii ambayo aghalabu hutokana na maisha katika jamii hiyo, wakati fulani kuliibuka neno fataki ambalo lilinasibishwa na wanaume ambao wanarubuni wanafunzi na kuwabaka au kufanya nao ngono.

Maana ya neno fataki ni karatasi inayotiwa baruti ili baadaye itegwe mahali kwa ajili ya kulipuka lakini maana hii ya nyongeza ilitumika kama misimu lakini baadaye ilikubalika katika jamii na kuingizwa katika kamusi ili itumike kama Kiswahili sanifu.

Misimu imekuwa ni mojawapo ya njia ya kuongeza msamiati katika jamii maneno mengi yaliyoanza kama misimu yameingia kwenye lugha sanifu. Hii imefanyika kwa sababu maana za maneno haya huelezea kwa usahihi kile kilichokusudiwa kusemwa.

Maneno kama kibaka kwa maana ya mwizi anayewaibia watu kwa kuwakwapulia linaelezea kwa usahihi aina ya wizi unaofanyika kuliko ungetumia msamiati mwingine.

Kashehe ni neno jingine ambalo lilianza kama msimu lakini kwa sasa limesanifishwa likiwa na maana ileile ya vurugu, zogo, fujo inayotokea mahali fulani.

Aidha, maneno mengine yameongezewa maana kutokana na kuibuka kwa maana za ziada kwenye msamiati huo.

Kwa mfano neno mzuka kwa maana ya ari na shauku baada ya kufurahishwa na jambo, maana hii imeongezewa kutoka maana ya msingi ya shetani anayempata mtu na kumfanya aseme mambo yasiyoeleweka.

MATATIZO YA MISIMU

Pamoja na kuwa misimu huongeza msamiati katika lugha kama tulivyoona, baadhi ya maneno ya lugha hii huchangia kukengeusha maana za msingi na kuwafanya watu kuchukia lugha hebu angalia maneno kujibebisha neno ambalo limeundwa kutokana na kutumia neno la Kiingereza baby na kulinyambulisha katika Kiswahili.

Misimu wakati mwingine hupunguza hadhira ya wapenda lugha ya Kiswahili kwa sababu kuna baadhi ya watu hawapendi lugha za matusi au zinazokera wengine. Sababu nyingine ambayo inaweza kuwa mbaya zaidi ni ile ya kubadilisha maana ya msingi ya maneno na kunasabishwa na matusi.

Kwa mfano maneno kama udenda au denda maana zake halisi katika Kiswahili sanifu zinajulikana kuwa ni mate au ute unaomtoka mtu pale anaposinzia bila kujitambua lakini siku hizi baadhi ya watu wamehamisha maana ya msingi na kulifanya neno hili kuwa tusi.

Neno jingine ni kazana ambalo hata kiongozi wetu mmoja wa kisiasa alithubutu kuwaambia Watanzania kuwa neno hilo ni matusi kwa sababu kulikuwa na maana ya msimu ambayo ilinasibishwa na matusi.

HITIMISHO

Misimu kama ilivyo vipengele vingine katika lugha kama tamathali za semi ni lugha ambazo haziwezi kuepukika kwa sababu binadamu si wakati wote anafanya shughuli zake kwa urasmi.

Wakati mwingine watu wanataka kujiburudisha baada ya kufanya kazi ngumu lakini pia wanataka kutaniana ili kufurahisha nafsi zao.

Kwa kutumia kipengele hiki cha misimu kuna nafasi kubwa ya kuendeleza au kuidunisha lugha yetu.

Jambo la kuzingatia ni kuwa kama misimu inaibuliwa na jamii na haiiathiri jamii hiyo kwa namna yoyote kipengele hiki cha lugha ya misimu kinahitaji kutafitiwa kwa kina ili kiweze kuchangia makuzi ya lugha kuliko kukibeza kwa kuona kila kinachoibuliwa katika misimu kinaonekana kuwa ni lugha ya kundi fulani. Kwa pamoja tuipende lugha yetu, tuienzi na tuitetee.

Mwandishi wa makala haya ni Mchunguzi wa Lugha Mwandamizi

BAKITA - 0712747199

Chanzo: habarileo.co.tz