KUNDI la Swahili Encounters linaloundwa na wasanii kutoka Zanzibar, Moroco, Ghana, Uingereza, Tanzania, Algeria na kuimba wimbo wa pamoja wamesema lugha ni changamoto wanayopata katika ushiriki wa kuimba kwa pamoja.
Wanamuziki hao huwa wanakutana siku tatu kabla ya Tamasha la Sauti za Busara kuanza linalofanyika Mji Mkongwe, Ngome Kongwe kisiwani hapa, hutanga wimbo mmoja unaohamasisha kauli mbiu ya tamasha hilo.
Wamesema changamoto wanayokutana nayo ni kwa kuwa wanakutana nchi nyingi, hivyo inachukua muda kuelewana hadi kukamilika wimbo.
Amina Omary maarufu Siti Amina kutoka Tanzania amesema kwakuwa muziki pekee yake ni lugha na hisia hivyo hutumia mbinu hiyo kukamilisha wimbo wa pamoja kutoka kila nchi.
“Ukweli hadi wimbo kukamilika huwa tunapata wakati mgumu sana kwa kuelewana sisi waimbaji, ila kwakuwa muziki ni hisia na ni lugha basi tunatumia njia hiyo kuelewana na kutoa kitu kizuri” alisema Sitti
Naye mwanamuziki Mehdi Laifaoui kutoka Algeria amesema kutoelewana lugha katika kushiriki kuimba wimbo wa pamoja kumesababisha mwaka huu kuwa na mwongozaji anayejua lugha za nchi tofauti tofauti ili kuwasaidia kuelewana.
Pia Soma
- Masanja anogesha Sauti ya Busara
- Watu kibao wajitokeza tamasha Sauti za Busara
- Sauti za Busara kumenoga, wasanii kila kona
“Kuna ugumu tunaoupata katika kutunga nyimbo ya pamoja kama unavyoona tunakutana nchi tofauti tofauti , uzuri mwaka huu tumepata muongozaji wa nchini tofauti na mwisho wa siku kukaa pamoja na kuelewana” alisema Mehdi
Kundi hilo la Swahili Encounters ambalo huwa linaundwa kipindi cha tamasha hilo huvunjika mwisho wa tamasha, wamesema huwa kila mwanamuziki mmoja anatunga kipande chake cha shairi na baada ya hapo huunganisha na kutoa wimbo kamili na mwaka huu wametoa wimbo unaoitwa ‘Sisi ni Sawa’ ambao unazungumzia kauli mbiu ya tamasha hili inayosema ni Paza Sauti, pinga unyanyasaji wa kijinsia.