Mwishoni mwa mwaka 2022, Alikiba kaonyesha kuchukizwa na kile walichokuwa anafanya Meneja wa Diamond Platnumz na WCB Wasafi, Sallam SK kwa kutoa kile alichoita orodha ya wasanii waliofanya vizuri mwaka 2022.
Katika orodha mbili za Sallam SK alimtaja Diamond kama msanii namba moja huku Alikiba akishika nafasi ya saba, hili ndilo likamuibua Kiba na timu yake na kusema huo ni mchezo wa kusaka kiki ila atabaki kuwa Mfalme wao.
Ikumbukwe Diamond na Alikiba wamekuwa wakitajwa kama washindani wakubwa kwenye muziki wa Bongofleva na mashabiki wa pande zote mbili wamekuwa wakichochea hilo kwa kiasi fulani kwa kujaribu kuwapambanisha.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba wasanii hawa kuna sehemu nyingi wametofauti katika muziki wao na mambo mengine yanayoshabiana na kazi yao iliyowapatia umaarufu. Je, yapi hayo?, karibu;
1. Maadili ya kazi (0 - 4)
Tangu anaanza muziki Alikiba hajawahi kufungiwa wimbo wake wowote na Baraza la Sanaa Taifa (BASATA), Kiba amewahi kusema hutengeneza muziki ambao hata mama yake mzazi anaweza kuusikiliza na video ambazo hata watoto wanaweza kuzitazama.
Hata hivyo, Diamond nyimbo zake mbili, Hallelujah na Waka zimefungiwa kutokana na kukiuka maadili, huku wimbo 'Mwanza' alioshirikishwa na Rayvanny ukifungiwa pia, na hata video ya wimbo wake 'Mtasubiri' aliomshirikisha Zuchu nayo imefungiwa!.
2. Albamu, EP (4 - 3)
Hadi sasa katika maisha yake ya muziki Diamond ametoa albamu tatu; Kamwambie (2010), Lala Salama (2012) na A Boy From Tandale (2018), huku akitoa na EP moja, First of All (2022).
Naye Alikiba ana albamu tatu sawa na Diamond ambazo ni; Cinderella (2007), Ali K 4Real (2009) na Only One King (2021) ila Kiba hana EP ingawa alitoka kimuziki kabla ya Diamond kwa zaidi ya miaka mitano.
3. Tuzo za Ndani (7 - 5)
Kwa zaidi ya miaka nane bado Diamond anashikilia rekodi ya kushinda tuzo saba za Muziki Tanzania (TMA) 2014 kwa usiku mmoja, Alikiba amejaribu kuvuja rekodi hii mara mbili bila mafanikio.
Mwaka 2015 Alikiba alikaribia kuivunja rekodi hiyo ya Diamond lakini akaishia kushinda tuzo tano pekee kwa usiku mmoja, mwaka jana ziliporeja tena tuzo hizo baada ya miaka saba, Alikiba alishinda tano pia, hivyo rekodi ya Diamond inaendelea.
4. Kazi na Baby Mama (2 - 0)
Alikiba amewahi kufanya kazi na wanawake wawili ambao wamewahi kuwa na mahusiano na Diamond hadi kujaliwa watoto ila Diamond hajafanya kitu kama hicho kwa Alikiba.
Alikiba alimtumia Tanasha Donna kutokea Kenya aliyejaliwa mtoto mmoja, Nasseb Junior, katika video ya wimbo wake, Nagharamia, pia alimtumia Hamisa Mobetto mwenye mtoto mmoja na Diamond, Dylan, katika video ya wimbo wake, Dodo.
5. Lebo Zao (2 - 0)
Lebo ya Diamond, WCB Wasafi inasimamia wasanii watano wakiwemo wawili wa kike, wakati Kings Music ya Alikiba ina wasanii wanne na hakuna hata mmoja wa kike.
Hata hivyo, kuna kimoja hapa wameenda sawa; kila mmoja kamsaini ndugu yake katika lebo yake, Diamond kamsaidini dada yake, Queen Darleen, huku Alikiba akifanya hivyo kwa mdogo wake, Abdukiba.
6. Tuzo za TMA (17 - 17)
Baada ya mwaka jana Alikiba kushinda tuzo tano za TMA alifikisha jumla ya tuzo 17 za TMA sawa na Diamond mwenye 17 pia, hata hivyo, Alikiba ameshiriki mara nyingi zaidi kwenye tuzo hizi.
Diamond ambaye na wasanii wote wa WCB Wasafi walijitoa katika tuzo za mwaka jana kwa kile walichodai kutoridhishwa na mchakato wake, yeye alifikia idadi hiyo mwaka 2015.
7. Lebo za Kimataifa (2 - 1)
Diamond amewahi kufanya kazi na lebo mbili kubwa za kimataifa ambazo ni Universal Music Group (UMG) na Warner Music Group ambayo yupo nayo hadi sasa.
Alikiba kafanya kazi na lebo moja, Sony Music ambayo mkataba ulishamalizika, huku akiwa hajatoa albamu chini yake, hii ni tofauti na Diamond ambaye albamu yake, A Boy From Tandale ilitoka chini ya Universal Music Group.
8. Kwenye soka (1 - 0)
Ukiachana na muziki, Alikiba ana kipaji cha kucheza soka na kashacheza hadi Ligi Kuu Soka Tanzania Bara mara baada ya kusajiliwa na Coastal Union FC kwenye msimu wa 2018/19 ingawa alicheza michezo michache.
Diamond naye anacheza soka ila hajawahi kufikia ngazi ya Ligi Kuu kama Alikiba ambaye karibia kila mwaka anacheza mechi ya hisani na mchezaji wa kimataifa Tanzania, Mbwana Samatta kupitia taasisi yao, SamaKiba Foundation.
9. Mapenzi na Kazi (0 -4)
Takribani miaka 20 katika Bongofleva, Alikiba hajawahi kurekodi wimbo na mwanamke yeyoye aliyewahi kuwa naye katika mahusiano au ndoa, hata kwenye video za nyimbo zake hilo halijawahi kutokea.
Ila Diamond kafanya hivyo na Tanasha Donna kupitia wimbo wao 'Gere' na Hamisa Mobetto kupitia wimbo 'Jibebe', pia Hamisa ndiye katokea kwenye video ya wimbo wake, Salome, huku Zari The Bosslady kwenye video za nyimbo, Utanipenda na Iyena.
10. Tuzo za Kimataifa (3 - 0)
Wasanii waliowahi kusainiwa WCB Wasafi yake Diamond wana mafanikio kimuziki kuliko wale wa Kings Music yake Alikiba upande wa tuzo za kimataifa ila ikumbukwe WCB ilianza kitambo kabla ya Kings.
Harmonize alishinda African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) 2016, Rayvanny alishinda BET 2017, huku Zuchu akiwa ameshinda tuzo mbili za AFRIMMA kama Msanii Bora Chipukizi (2020) na Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki (2022).