Kweli hujafa hujaumbika, leo mzima kesho kitandani. Hii imemkuta Meneja wa bendi ya Akudo Impact ‘Vijana wa Masauti’, Ramadhani Pesambili ‘Rama Akudo’, ambaye kwa sasa yuko kitandani akipigania uhai wake baada ya kufanyiwa operesheni tatu.
Mwanaspoti ni mdau mkubwa wa burudani na lilimtembelea nyumbani kwake Mwananyamala Komakoma maeneo ya Kopa Kabana jijini Dar es Salaam ili kufahamu tatizo lililomkumba na anasema alianza kuumwa akiwa Dodoma kwenye shoo ya Akudo Impact Februari mwaka jana, ambako alihisi mguu kama umestuka na kupata maumivu makali. Hata hivyo, baada ya muda yalipungua na kurudi Dar es Salaam akiwa salama kabisa.
“Sasa kuna siku nimetoka katika matembezi yangu, nikiwa narudi nyumbani nikafika Mwananyamala A, nikaona kama mguu umepigwa shoti, nikawa nashindwa kutembea, nilitulia kidogo, mara akatokea rafiki yangu mmoja akanipa msaada wa kunikokota hadi kunifikisha nyumbani kwangu. Huwezi kuamini, nilitumia takriban saa tatu hadi kufika ilhali hapo Mwananyamala A hadi kwangu ni mwendo wa dakika tano tu. Nilipofika nyumbani yule rafiki yangu aliyenisindikiza akanishauri niende hospitali. Tukaenda Hospitali ya Taifa Muhimbili. Baada ya kupata matibabu majibu yalikuja kuwa nimegundulika nina usaha kwenye nyonga, nikapewa dawa za kutumia. Hali ikazidi kuwa mbaya ndipo nikafanyiwa upasuaji kwenye nyonga na kutolewa usaha nusu kisado.”
Rama Akudo ambaye alianza umeneja katika bendi ya Akudo mwaka 2012, aliongeza; “Baada ya upasuaji huo wa kwanza, nilipata nafuu kidogo tofauti na yale maumivu ya mwanzo niliyokuwa nayasikia. Lakini kadri siku zilivyozidi kwenda hali ilibadilika tena ikabidi nipelekwe Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Tawi la Mloganzila iliyopo Mbezi ya Kimara jijini Dar es Salaam, pale nilianza kuchukuliwa vipimo upya. Wakachukua kinyama sehemu ya nyonga na kuambiwa nisubiri majibu baada ya wiki. Lakini kila nikifuatilia majibu ikawa naambiwa bado-bado, ndipo nikaamua kwenda hospitali nyingine ya Ibrahim Hajj iliyoko Posta jijini Dar es Salaam baada ya kuona majibu yangu yanachelewa na maumivu yanazidi.
“Hapo Ibrahim Hajj nilipata vipimo na kuambiwa natakiwa kufanyiwa upasuaji ili nikamuliwe tena usaha, hivyo sikuwa na ubishi kwani maumivu niliyokuwa nayapata Mungu ndiyo anajua, hiyo sasa ikawa ni upasuaji wa pili. Kiukweli ilikuwa kila nikikamuliwa usaha ndiyo napata nafuu.
“Sasa nikawa najiuliza, haya maisha ni hadi lini? Nimekosa nini mimi maana hata ugonjwa sijui ninachoumwa daah! Sijui kwa kweli uhai wangu mimi Rama Pesambili. Ila baada ya kutolewa huo usaha tena nikawa naendelea na matibabu lakini maumivu yalikuwa yanazidi kadri siku zinavyozidi kwenda na miguuni nikawa nakosa nguvu hata ya kutembea, siku moja nilizidiwa sana nikarudishwa hospitalini tena.
“Nilirudishwa katika hospitali ya Ibrahim Hajj ambao walinifanyia upasuaji wa pili. Nilipofika wakanilaza na kuanza kuchukua vipimo na kuendelea na dawa. Majibu yao walikuja kuniambia kuwa natakiwa kufanyiwa upasuaji mwingine wa kukatwa korodani moja, niliumia sana na kuyasikitikia maisha yangu, kwa nini chanzo cha kichomi na mguu kushtuka yamefika hapa! Kiukweli niligoma lakini baada ya muda maumivu yalizidi kuwa makali, ikabidi nikubali kutolewa korodani moja, hapa kwa sasa nimebaki na korodani moja.”
Rama Akudo anasema tangu aondolewe korodani moja, hali yake imekuwa na nafuu yaliyobaki ni maumivu ya mguu tu, ambayo kwa sasa anatembelea magongo.
“Nina nafuu, japo maumivu yaliyobaki ni kwenye mguu ambao umesababisha kwa sasa natembelea magongo, na hivi ulivyonikuta ndio maisha yangu nashinda ndani tu na muda mwingi nalala kwa ajili ya kunyoosha miguu,” anasema.
“Niwe tu mkweli, sina kitega uchumi chochote ninachotegemea kupata pesa zaidi ya misaada kutoka kwa watu wangu wa karibu. Nilipoanza kuumwa Mh. Kapuya alitoa pesa za kufanyiwa upasuaji mara ya kwanza na siku zilivyoendelea kuna kundi moja la muziki wa dansi linaitwa Cheza Kidansi lilijichangisha pesa na kunipatia. Pia kuna mdau mmoja wa muziki wa dansi, Jimmy Kamuzora, alikuja kunitembelea hapa nyumbani na kuniachia pesa. Wapo watu wananipa msaada japo wengi hawajui kama naumwa, ila nadhani wakiona wewe ukienda kuandika gazetini, ndio watajua, sababu hakuna mwandishi yeyote aliyekuja kuniona.
Rama Akudo anasema watakaoguswa na hali ngumu anayopitia hivi sasa watamfariji sana kama wakimchangia ili aweze kuendelea kupambana kujaribu kuokoa maisha yake.
Tangu ameanza kuumwa, Rama Akudo anasema anauguzwa na kaka yake ambaye ametoka Tabora, akishirikiana na mke wake, ambaye wamejaaliwa kupata mtoto mmoja. Siku Mwanaspoti lilivyoenda nyumbani kwake lilimkuta kaka yake akimhudumia.
Atimkia Tabora
Wiki moja baada ya mahojiano na Mwanaspoti, Rama alilipigia simu Mwanaspoti na kutaarifu amesafiri kwenda nyumbani kwa Mh Kapuya, Tabora Wilaya ya Kaliua kwa ajili ya kwenda kuugulia huko.
“Mimi naomba tu kitu kimoja kwa watu wangu wote wa karibu, wadau wa muziki wa dansi na hata wasio karibu na mimi wala wasio wadau wa dansi, kinachoendelea kuhusu afya yangu, wazidi tu kuniombea ili nirudi katika hali yangu ya kawaida na kwa watakaoguswa na kutaka kunipatia msaada basi watume tu kwenye namba hizi 0715-862051 hii ni Tigo na Voda ni 0764888840 jina ni Rama Pesambili. Mungu aendelee kuwabariki sana na naomba maombi yenu,” anasema Rama Akudo.