Mwonekano wa mwanamke ni silaha tosha. Unatumika wakati gani na kwa madhumuni gani huo ni mjadala mwingine.
Wakati watu wakipoteza maisha katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia na madhara mengine ya kibinadamu yakitokea ikiwamo mali kuteketea, jambo jingine ambalo linaweza kuonekana la ajabu au la kipuuzi lilijitokeza. Jambo hilo ni malalamiko ya wanawake kutokana na kuadimika kwa vipodozi.
Wakati ule ukimuuliza mwanamke ni kitu gani kiliathiri maisha yake wakati wa vita hiyo japo kuna matukio atakayoyataja lakini mojawapo ni kukosekana kwa bidhaa hiyo muhimu.
Miaka 74 baadaye urembo haujawaacha wanawake salama. Kilichobadilika ni namna wanawake walivyopiga hatua katika kufanya chochote ili watimize azma ya kupata mwonekano wanaoutaka.
Mkorogo, vigodoro, vipodozi, kucha, kope na nywele bandia ni sehemu ya maisha ya wanawake wengi.
Uchunguzi wa mwandishi wa makala haya alioufanya kwa wanawake wenyewe na watalaamu unaonyesha kuwa wanawake wanapenda kujipodoa na hali hiyo inatokana na asili ya kimaumbile.
Wanawake waliohojiwa walikuwa na sababu tofauti za kufanya hivyo, 15 walisema wanataka waonekane warembo maana mwanamke aliumbwa kuwa kivutio, wengine 14 walisema wanafanya hivyo kuwafurahisha wanaume maana wanapenda wanawake warembo.
Wanawake wengine 10 walisema wanawake wanaofanya hivyo sababu kubwa ni ulimbukeni, kutojitambua na mashindano huku wengine sita wakisema wanafanya ili kuwanasa wanaume kirahisi katika hisia za kingono (wanafanya biashara).
Shirika la Utafiti la Sayansi ya Jamii Afrika (CODESRIA) mwaka 2016 lilifanya mkutano wa majadiliano kuhusu jambo hilo ambapo washiriki kutoka nchi 13 walisema wanawake wanafanya hivyo kwa sababu wanataka kujiongezea kujiamini.
Sababu nyingine zilitajwa kuwa ni mwingiliano wa utamaduni wa nchi za kigeni na imani potofu kuamini kwamba, wanaume wengi wanapenda wanawake weupe, wenye makalio makubwa na wenye kujipamba kwa kubandika kope, wigi na kucha bandia licha ya suala hilo kukanushwa na baadhi ya wanaume huku wakisema hawapendi kabisa mambo hayo kwa wanawake.
Viongozi wa dini walipoulizwa sababu za ongezeko la utamaduni huo walisema katika misingi ya kiimani kufanya hivyo ni kumtukuza shetani, kukosoa uumbaji wa Mungu maana Mungu alimuumba mtu kwa uzuri na upendeleo wa ajabu.
Padri wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Manzese jimbo la Dar es Salaam, Paulo Sabuni alisema, “Mwanamke unapouharibu mwili kwa kuweka vitu bandia unaukosoa uumbaji, unamwambia Mungu ulikosea kuniumba hivi ulipaswa kuniumba hivi wakati tunaambiwa Mungu alimuumba mtu kwa namna ya kupendeza,”anasema.
Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislam Tanzania, Sheikh Khamis Mataka alisema kujibadilisha maumbile na muonekano kwa vitu bandia ni kumtukuza shetani maana katika maandiko yanakataza.
Mchungaji wa Kanisa la The River of Healing, John Kyashama alisema kwa kuanza kunukuu baadhi ya maneno katika kifungu cha biblia akisema: “Wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri na adabu nzuri na moyo wa kiasi, si kwa kusuka nywele wala kwa dhahabu na lulu wala nguo za thamani bali kwa matendo mema.
Utafiti wa Profesa Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Georgia, Atlanta, Marekani, Kelly Lewis wa kitengo cha Sosholojia, kuhusu wanawake unasema kuna idadi kubwa ya wanawake Tanzania wanatumia ‘mkorogo’ na huenda wakaugua saratani, kuzaa watoto wenye mtindio wa ubongo au kupoteza maisha kutokana na kukithiri kwa matumizi ya vipodozi vyenye kemikali hatari.
Gazeti hili pia limezungumza na wanaume ili kujua kama kweli wanavutiwa zaidi na wanawake wanaobadili muonekano, kati ya wanaume waliohojiwa walisema hawavutiwi kwa sababu urembo uliokithiri huwakera.
“Kwa upande wangu siungi mkono mwanamke anayefanya haya,” alisema Elias Peter mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam.
John Ephrahim mkazi mwingine wa Tabata alisema, “Wanawake wa aina hiyo hawawezi kuwa kivutio kwangu hata siku moja, maana napenda uhalisia. Urembo hauleti uzuri bali uzuri ni asili. Ubaya ni kwamba sasa hivi kila mmoja fikra yake ni kutaka kujibadili kutoka kwenye uzuri na kuja kwenye urembo,” alisema.
Mjasiriamali wa masuala ya urembo kutoka Makumbusho, Dar es Salaam, Tulanana Jilo alisema wanawake wengi wanafanya hivyo ili kutaka kuonekana mbele za watu kuwa wana maisha mazuri, mashindano na kukomoana.
“Kuna mawili wapo wanaofanya hivyo kwa kuwa wanataka waonekane ama waonyeshe jamii inayowazunguka kuwa hata wao ni wazuri na wanajiweza kifedha, wapo wanaofanya hivyo kibiashara kwa maana wanatangaza soko”.
Paulina Msangi mkazi wa Manzese, Dar es Salaam alipoulizwa alisema wanaume ndiyo chanzo cha haya kwani hapo nyuma walikuwa wanapenda wanawake weupe na wenye makalio makubwa hivyo wanawake wakaona kitu muhimu ni kubadilisha ngozi na kuwavutia.
“Wengi tunatafuta mvuto, tunaamini tusipojipamba hatupendezi na kama inavyofahamika kuwa mwanamke ni ua tumeumbwa kuwa kivutio machoni mwa wanaume,” alisema Irene Petro mkazi wa Mwenge, Dar es Salaam.
Aliongeza, “ndiyo maana wanawake tunafanya namna yoyote ili tujiweke namna ambayo tutavutia, sasa katika kujiweka huko wengine wanajikuta wanaharibu na kuzidisha badala ya kuvutia anakuwa kituko,” alisema.