Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa Diamond tunaiona tofauti ya usanii na uwekezaji kwenye sanaa

64802 Diamond+puic

Sat, 29 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Julai 12, tamasha la Wasafi litaanza kutimua vumbi la burudani likianzia wilaya ya Muleba mkoani Kagera.

Hii inaweza kuwa siyo habari mpya kwa sasa, kipya ni namna staa kutoka lebo ya WCB, Naseeb Abdul maarufu kama Diamond anavyojitofautisha na wasanii, usanii na uwekezaji katika sanaa.

Diamond amefanya uwekezaji kwenye sanaa na sasa anakula matunda ya alichokiwekeza katika sanaa.

Katika tamasha kama hili msimu uliopita yaani mwaka 2018 alifanya tamasha kama hilo na kuzunguka kwenye mikoa kadhaa ikiwamo Iringa, ambako ni miongoni mwa maeneo matatu anayoanza nayo mwaka huu ukiachilia Muleba na Tabora, alikwenda pia Morogoro, Mtwara na kumalizia nchini Kenya.

Kwenye tamasha hilo la mwaka jana Diamond akiwa nchini Kenya alitumia wasanii aliowazalisha kwenye lebo yake na kumuongeza Navy Kenzo pekee.

Hii inaonyesha kwamba amevuna matunda ya uwekezaji kwenye eneo la kuzalisha wasanii na kuwatumia baadaye.

Pia Soma

“Kumchukua msanii na kumfanya awe staa katika muziki ninaweza na nina nyenzo nyingi za kulifanikisha hilo, lakini kwanza msanii huyo awe anajibeba yeye mwenyewe.

“Kung’aa ukiwa WCB si habari mpya sana, habari mpya ni namna wewe unavyoweza kuendana na mazingira ya lebo yangu, lazima ujitume sana ili utofautiane na wengine ukifanya hivyo kukuuza sokoni inakuwa kitu rahisi “anasema Diamond akizungumzia sifa za wasanii wanaostahili kufanya kazi na lebo yake.

Kwa maana hiyo Diamond anaweza kuzunguka Tanzania nzima akifanya tamasha la Wasafi akitumia wasanii kutoka katika lebo yake na asichokwe na mashabiki kwa sababu amewekeza kwao na wao wamewekeza kwake.

Staa huyo pia ana manukato maarufu yajulikanayo kama Chibu perfume.

Uwekezaji mwingine huo ambao utampatia fedha kupitia tamasha hilo.

“Kila mkoa tutakakopita tutakuwa tunatangaza awamu ya pili ya manukato haya, awamu ya kwanza ilikwisha mapema,” anasema.

Unaweza kuona mbali ya burudani ya muziki atakayotoa lakini kupitia ushawishi wa sanaa yake pia ataweza kuuza manukato yake.

WCB pia kuna mavazi ya aina mbalimbali yenye lebo zao ikiwamo kofia, fulana na majaketi.

“Kila mkoa tutakaopita kutakuwa na maduka maalumu ya kuuza nguo zenye lebo ya WCB.

“Lengo letu ni kuhakikisha kabla ya kuingia uwanjani kushuhudia shoo kali kutoka kwetu, mnakuwa mmechafuka kwa nguo za WCB,” anasema Diamond.

Kwa mikoani bila shaka wako watakaohamasika na kununua nguo hizi ili mtu akiingia kwenye shoo hiyo naye awe kama mmoja wao.

Kwa hivyo mbali ya fedha ya kiingilio, Diamond pia atavuna fedha ya mauzo ya bidhaa kutoka kwenye lebo hiyo.

Mbali na kituo cha matangazo cha Wasafi TV, mkali huyo ambaye kwa sasa anatamba na kibao chake kipya cha ‘Kanyaga’ ni miongoni mwa wamiliki wa kituo cha matangazo cha redio kiitwacho Wasafi FM.

Hii nayo ni aina nyingine ya uwekezaji katika muziki, kwa sababu wakati wa tamasha hilo pia watakuwa wakizindua masafa ya redio hiyo katika baadhi ya mikoa watakayopita.

Licha ya meneja wake Said Fella kulalamikia kupata shida ya wadhamini, bado uwekezaji wa Diamond kwenye sanaa umemsaidia kupata wafadhili si haba, tamasha lenye miaka mitatu kuwa na wadhamini wasiopungua watano, wengine wakiwa nao mara zote.

Hii ni aina ya uwekezaji kwenye kitu unachokijua na kukipenda, anaonyesha kabisa kupitia sanaa amekuwa mwekezaji kwa ajili ya maisha ya baadaye.

Inawezekana kabisa Diamond asiimbe lakini kwa uwekezaji wake katika sanaa akaendelea kula kwa kutengeneza fedha kupitia kazi zake.

Hana masihara anapotayarisha kazi zake, ina maana baadhi ya kazi hizo zinaweza kuendelea kumuingizia fedha miaka kadhaa ijayo, hilo si jambo la kubeza hata kidogo.

Ninasisitiza, wasanii kumbukeni kuna kesho, wale ambao mmejipanga kwa hilo hongereni sana, wale mnaosuasua wakati ni sasa.

Ni vyema mkaanza sasa kutofautisha sanaa na usanii, tofuati ya hilo itajidhihirisha pale mtakapoanza kuwekeza kikamilifu kupitia kwenye sanaa.

Chanzo: mwananchi.co.tz