HUZUNI imetanda kila kona kuhusiana na kifo cha mtoto Patrick aliyefariki juzi wakati akipatiwa matibabu kwenye hospitali moja jijini Nairobi, Kenya.
Patrick (8) ambaye alikuwa akiishi kistaa na kuwa na umaarufu wa aina yake kwenye mitandano ya kijamii, hasa baada ya kuokoka, amekuwa akifuatiliwa sana na kifo chake kimeumiza wengi. Mtumiaji gani wa Instagram ambaye hakuwa akimfahamu na kufuatilia matukio mbalimbali ya Patrick? Dogo alikuwa na wafuasi wengi mtandaoni, lakini ghafla tu amezimika. Inatia huzuni sana.
Hata hivyo, mengi yameanza kufumuka baada ya kifo cha Patrick, ambaye ni mtoto wa staa wa kike, Rose Alphonce ‘Muna Love’, ambaye alikuwa akimuuguza hospitalini hadi alipokutwa na umauti.
Lakini, wakati ndugu, jamaa na mashabiki wakisubiri mwili wa Patrick kuletwa nchini kwa shughuli zingine za mazishi, utata wa mahali ambapo msiba utakuwepo ukashika kasi. Awali, ilielezwa kwenye mitandao kuwa msiba utakuwa nyumbani kwa Muna kule Mbezi Beach.
Wakati utata huo ukiendelea, dada wa Muna, Eve akaibuka na kueleza kuwa msiba wa Patrick utakuwa nyumbani kwa baba yake, Peter Zakaria anayeishi Mwananyala kwa Mwakibile, Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwanaspoti, Eve anasema wameamua kuweka msiba Mwananyamala kwa sababu ndiko nyumbani kwa baba yake Patrick.
“Msiba hauko huko Mbezi jamani, Patrick ana baba yake yuko hai anaitwa Peter, hivyo tuko hapa Mwananyamala kwa Mwakibile na hapa tunapanga jinsi ya kuleta mwili nchini kwa ajili ya taratibu za maziko. Bado hatujapanga siku rasmi ya kuzika, lakini mwili utakapoingia kila kitu kitakuwa wazi,” alisema.
Pia, aliwataka watu kuacha kusambaza habari za kupotosha kwenye mitandao na kwamba, kama wanataka ukweli wafike msibani.
Kuhusu kifo cha Patrick, Eve alisema ameugua kwa wiki mbili akisumbuliwa na matatizo ya kichwa yaliyotokana na kuwa na uvimbe kichwani.
“Nimetudi jana tu kutoka hospitalini Nairobi ndipo huku nyuma yanatokea haya. Tulimepeleka Nairobi kwa ajili ya matibabu ya kichwa, kilikuwa kinamuuma kila wakati hivyo, kuweka uvimbe ila ndio hivyo Mungu amempenda zaidi.
Pia, amesema kuwa taarifa za kwenye mitandao kuwa Patrick ni mtoto wa mtangazaji wa Clouds FM, Casto Dickson hazina ukweli na kuwa, baba wa mtoto ni Peter.
“Watu wasipende kuzungumza mambo wasiyoyajua, Caston sio baba wa Patrick kama inavyodaiwa, hivyo watu waachane na hizo ishu za mitandaoni,” alifunguka Eve.
Mastaa wamlilia Patrick
Achana na umaarufu alionao akiwa bado mdogo kabisa huko kwenye mitandao ya kijamii kutokana na staili yake ya kupiga pamba na staili za nywele, lakini Patrick amekuwa maarufu zaidi kutokana na kile kilichoelezwa kuwa amefuata wakovu. Japo ni mtoto lakini matendo na kauli zake zilieleza bayana kuwa, amefuata wakovu na jamii imchukulie hivyo.
Jamii hasa tasnia ya Bongo Flava, Bongo Movie na viongozi wamepokea taarifa za kifo cha Patrick kwa mshtuko mkubwa, ambapo salamu zilianza kumininika kutoka kila kona. Huko kwenye mitandao ya kijamii ndio kukachafuka kwelikweli kila mmoja akielezea kuguswa na kifo hicho.
Kamanda mwenye mkoa wake, Paul Makonda aliweka video kwenye ukurasa wake wa Instagram ikimuonyesha Patrick akisali kisha kueleza kuwa, amempokea Yesu. Makonda akionekana kuguswa na kusema: Hata sijui cha kusema. Faraja yangu ni juu ya mtoto huyu katika maisha yake alimjua Yesu. Mungu akupokee uncle wangu”.
Mbali na Makonda, wasanii mbalimbali waliposti picha na video za Patrick kisha kuandika ujumbe wa majonzi kuelezea hisia zao akiwemo, Ali Kiba, Wema Sepetu, Diamond Plutnumz, Hamisa Mobetto, Irene Uwoya, Snura, Jux, Tunda Man, Khadija Yusuf, Zari, Ray C, Dr Cheni na Banana Zoro,
Enzi za uhai wake, Patrick alimshawishi mama yake kuachana na mambo ya dunia na kuingia katika wokovu, baada ya kuumwa mguu uliosababishwa na nyonga kusagika, ambapo alitibiwa na kupona.
Muna mwenyewe aliwahi kukiri mbele ya Mwanaspoti kuwa, ameamua kuokoka kutokana na mitihani mikubwa aliyopitia Patrick.
Mwaka juzi, Patrick alianza kuumwa mguu kama utani na baada ya kwenda Hospitali iligundulika kuwa amesagika sehemu ya maungio ya mguu wake wa kulia.
Katika kuugua huko alianza kwa kutambaa, lakini awali hakuamini kama ni kweli kwani huko nyuma alikuwa akimsumbua kumtaka mdogo wake, hivyo akaona kama anaigiza tu.
Lakini, hali ilikuwa tofauti kwani iliendelea kwa siku tatu mfululizo ambapo alishindwa kabisa kutembea na alipojaribu kufanya hivyo, alishindwa na kumfanya kuchechemea kwa shida.
Hapo ndipo aliposhtuka na kuanza kukimbizana kwenye hospitali akitafuta tiba na baadaye iligundulika kuwa ana tatizo la kusagika maungio hivyo kusababisha mfupa kusagika.
Katika kusaka tiba ya matibabu hayo, Patrick alifanyiwa upasuaji kwenye Taasisi ya Mifupa (MOI) na baadaye ilishauriwa awekewe madini ambayo gharama yake ilikaribia Sh50 milioni ili kumwezesha kutembea kawaida.
Hata hivyo, wakati matibabu hayo yakiendelea, Patrick alikuwa akisisitiza kutaka kuokoa kwa kuwa, anaamini ndio utakuwa mwisho wa tatizo hilo na atapona kabisa.