Mara nyingi inapotokea umejeruhiwa penzini hususan kwa mtu ambaye ulikuwa na malengo naye ni vigumu sana kupenda tena.
Ni vigumu sana kumuamini tena mtu wa jinsia tofauti na yako. Wakati mwingine unaamini mtu wa jinsia ya tofauti na yako ni kama muuaji, ni mtu asiyestahili kuwa karibu yako.
Ndugu zangu, tunakosea. Haya yote yanatokea kwa sababu. Japo hakuna anayeyafurahia lakini endapo yakitokea, usihu-zunike. Chuk-ulia kama chang-amoto na amini utasi-mama tena.
Sahau mapito yako. Elewa kwamba aliyekutenda hilo, wakati wewe unaumia yeye hana habari na wewe. Kwa nini uumie kwa sababu yake, kataa kuumia. Maisha mazuri kwako yapo. Amini furaha yako ipo mbeleni, itachelewa tu lakini inakuja. Mtu sahihi yupo tu wala usiumie moyo.
Chukulia kuachwa kwako kama somo. Ukweli ni kwamba wakati mwingine tunapaswa kuanguka ili tuweze kusimama upya.
Kujifunza kutokana na makosa yako ya zamani ni njia pekee ambayo unaweza kujiongoza kupata upendo unaostahili badala ya kufanya makosa tena.
Usimchukie aliyekuacha maana huwezi kujua mngeendelea naye angefanya nini juu ya maisha yako. Yawezekana angekuja kuwa tatizo huko baadaye. Yawezekana angekuja kuwa mwiba au sumu katika pendo lako wakati tayari mpo kwenye ndoa. Mpende, mruhusu aende, usimchukie. Muombee heri huko aendako. Mchukulie aliyekuumiza hakuwa mbaya bali hakuwa tu mtu bora kwako.
Jiweke kwenye wakati mzuri wa kuruhusu moyo wako upende tena. Maisha lazima yaendelee, aliyekuumiza anapenda tena huko aliko, kwa nini wewe usipende tena? Utaumia mpaka lini? Utahuzunika hadi lini, kataa huo utumwa.
Jiamini kwamba wewe ni bora, amini kwamba kilichotokea hadi ukaachwa ni changamoto tu. Usitafute mchawi. Amini kwamba unaweza kuingia kwenye uhusiano mwingine na ukasahau kabisa maumivu uliyoyapitia.
Mapenzi siku zote ni hatari. Kumkabidhi mtu moyo wako ni jambo linalohitaji imani ya hali ya juu. Baada ya kuishi huru muda mrefu, chukua nafasi ya kumpa mtu nafasi nyingine ya kuanzisha naye uhusiano. Ruhusu moyo wako upende tena na ujifunze kutokana na mahusiano uliyoyapitia.
Kama kuna mahali unahisi ulikosea, ni wakati wa kujirekebisha na kusimama upya. Tafuta furaha ya moyo wako. Usikubali moyo wako uishi kwenye majonzi. Hakikisha unaisaka furaha yako, upe amani moyo wako kwa kuzungumza na watu sahihi, watakaokupa furaha kila siku badala ya karaha.