Julai 4 mwaka 1776 taifa la Marekani lilipata uhuru kutoka kwa mkoloni taifa la Uingereza. Kisha miaka 188 baadaye ndipo taifa la Tanzania liliundwa kwa muungano wa mataifa mawili machanga, Zanzibar na Tanganyika.
Miaka 188 ni mingi sana. Kwa kukupa picha rahisi tu ili uelewe ni kwa kiasi gani miaka 188 ni mingi, fikiria kwamba, wote, mimi na wewe hatutaishi miaka 188 hapa duniani. Na ikitokea mmoja wetu akafikisha miaka hiyo basi ni lazima atakuwa kama makumbusho, watu watalipia pesa kumuona.
Kwa wastani wa maisha ya binadamu kwa sasa, miaka 188 inaweza kutengeneza vizazi mpaka vinne. Yaani wewe, utapata mtoto, kisha mtoto wako atapata mtoto wake, mtoto wake atapata mtoto wake. Hiyo ndiyo miaka 188. Miaka 188 inatosha kugundua simu, kugundua intaneti, kamera, gari, ndege, mashine za kutotoleshea kuku, mashine za kukamulia ng’ombe maziwa.
Yaani miaka 188 inatosha kabisa kugundua kompyuta, mashine za MRI na CT scan zinazotumika mahospitalini, gari zinazotembea zenyewe, mashine za kuchapisha magazeti, televisheni, radio na hata bluetooth.
Yaani miaka 188 inatosha kugundua ugonjwa wa Uviko 19 na kinga yake, kugundua tiba ya malaria, kifua kikuu na vitu vingi sana. Yote hayo ni kukwambia kwamba, miaka 188 ni miaka mingi kinoma.
Sasa kwa sababu miaka 188 ni miaka mingi, sidhani kama ni haki sisi kama taifa kujilinganisha na taifa lililotutangulia miaka 188 kwa namna yoyote ile.
Yaani sisi Wabongo hatutakiwi kujilanganisha na Marekani kielimu, kisayansi, kimipango, kijamii, yaani hatutakiwi kujilinganisha nao kabisa kwenye kitu chochote kile, labda tu kwenye ukweli wa kwamba sisi na wao sote ni binadamu, lakini kwenye vitu vingine vyote tunakosea kujilinganisha nao.
Kwahiyo kama tunakosea kujilinganisha nao kwa namna yoyote basi ni sawa kabisa na kusema tunawakosea wasanii wetu kuwalinganisha na wasanii wa Marekani hususan kwenye vitu vinavyohusisha teknolojia.
Ndiyo maana nawashangaa watu ambao baada ya kuona shoo ya Rihanna iliyofanyika kwenye Super Bowl majuzi wanaanza kuuliza mbona wasanii wetu hawafanyi mambo kama yale?
Yaani eti wanataka Zuchu apige shoo kama zile, za kupaa juu juu ambazo unaandaji wa jukwaa umefanyika ndani ya dakika tatu kama sio saba, chap kwa haraka yaani. Aisee, huko ni kumkosea heshima Zuchu na wasanii wote Bonge.
Tunapenda wasanii wetu wawe na maendeleo kwenye sanaa zao lakini ukweli useme, kama tutaendelea na tabia ya kujilinganisha na watu waliotutangulia kwenye gemu kwa miaka 188 lazima tutaendelea kujiona kama vile hatuendelei, hatuna tunachokifanya. Wakati kiuhalisia ni kwamba, tunafanya vizuri kwa kasi yetu.