Msanii wa muziki kutoka nchini Nigeria Oluwatobiloba Daniel Anidugbe maarufu kama Kizz Daniel amezungumza na wanahabari jana Jumanne, Agosti 9, 2022 katika hotel ya Rotana na kuwaomba radhi mashabiki zake na Watanzania wote kwa ujumla kutokana na kushindwa kufanya shoo nchini.
Hitmaker huyo wa ngoma ya Buga amesema hayo ikiwa ni siku mbili baada ya kudaiwa kukacha shoo ya Summer Amplified aliyotakiwa kufanya usiku wa kuamkia Agosti 8, 2022 katika Ukumbi wa Warehouse Nextdoor jijini Dar, jambo lililosababisha kukamatwa na polisi na kuhojiwa.
Mbali ya kuomba rqdhi, Kizz amesema atarudia kufanya shoo yake siku ya Ijumaa huku waandaaji wa shoo hiyo wakieleza kuwa watataja sehemu ambapo shoo hiyo itafanyika na itakuwa bure kwa waliokuwa wamekata tiketi tangu awali.
“Kwanza niombe radhi Watanzania kwa kilichotokea. Nilikuwa na shoo Kampala nchini Uganda, nikaondoka nilipofika Nairobi Kenya ndege niliyotakiwa kuunganisha nayo kuja Tanzania nilikuta imeshaondoka.
"Nilikaa Nairobi kwa saa nane, nikapata ndege ya kuunganisha saa mbili na nusu usiku. Nilipofika Dar tukagundua kuna vitu vyangu muhimu na vingine ni vya shoo vimesahaulika Nairobi na vingi vilikuwa muhimu kwa ajili ya shoo, wakasema watanitumia.
"Nilipofika ilikuwa usiku sana nikafikia hotelini, nikaambiwa nikafanye sound check lakni kutokana na mazingira tayari mashabiki walikuwa wameshajaa ukumbumbini, ingekuwa ngumu kwangu, tutakubaliana na waandaaji ikaenda bendi yangu kufanya sound check kwamba nitapiga shoo kwa vifaa hivyohivyo vilivyopo, lakini mazingira hayakuwa rafiki kwa sababu tayari mashabiki walikuwa wameshasubiri vya kutosha, wamechoka na wengine wamekasirika, kwa busara nikaona itakuwa ngumu kufanya shoo katika hali ile.
"Mchana polisi walikuja wakanichukua pale hotelini nilipofikia, si kwa lengo la kunikamata kama baadhi ya watu wanavyosema bali kwa ajili ya kuchukua maelezo yangu nini kilitokea.
“Hata hivyo nilikaa na promota na wandaaji tukakubaliana kwamba tufanye kitu kwa ajili ya mashabiki na tukakubaliana kwamba shoo lazima iendelee, itafanyika Ijumaa wiki hii. Naomba radhi kwa mashabiki, sikukusudia kufanya hivi, sikuwa na lengo la kuwaudhi.
“Naipenda kazi yangu, nilikuja kutumbuiza na ninakusudia kutumbuiza. Ni matumaini yangu kwamba mtanipa nafasi nyingine ya kutumbuiza Ijumaa," amesema Kizz Daniel.