Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiswahili kutumika mikutano Benki ya Dunia na IMF

Dkt. Saada Mkuya Dkt. Saada Mkuya.

Tue, 17 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tanzania imeishauri Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kukifanya kiswahili kuwa miongoni wa lugha za mawasiliano wakati wa mikutano yake kutokana na kukua kwa lugha hiyo na kutumika kwenye mikutano mingine mingi ya Kikanda na Kimataifa.

Ushauri huo umetolewa Mjini Marrakesh nchini Morocco, na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya wakati wa Mkutano wa 26 wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika ambazo ni wanachama wa Benki ya Dunia.

Dkt. Saada Mkuya Salum amesema kuwa ni wakati muafaka wa kukijumuisha Kiswahili katika mijadala ya Taasisi hizo kubwa za Fedha duniani kwa kuwa wanachama wake wengi kutoka katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara wanazungumza lugha hiyo.

“Takribani watu milioni 200 wanazungumza Kiswahili duniani, tumewasilisha ombi hili ikiwa ni jitihada za Serikali za kukibidhaisha Kiswahili saw ana lugha nyingine zinazotumika kama lugha rasmi kwenye mikutano ya Benki ya Dunia na IMF), alisema Dkt. Saada Mkuya Salum.

Agenda hiyo itajadiliwa wakati wa Mkutano wa 27 wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika ambazo ni wanachama wa Benki ya Dunia, wakati wa Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) itakayofanyika Washington D.C, nchini Marekani Mwezi Aprili Mwakani.

Aidha katika mkutano huo wa 26 wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika, wajumbe waliiomba Benki ya Dunia kutoa fedha kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa kuwezeha biashara ya hewa ukaa, kusaidia bajeti za nchi wanachama na kuongeza kiwango cha fedha za mikopo nafuu na misaada kwa nchi zinazoendelea kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Waliitaka pia Benki hiyo kuzihudumia nchi wanachama wake kwa usawa wakati wa majanga ikiwemo matatizo ya mizozo ya kivita kama wanavyofanya kwenye nchi nyingine zenye matatizo kama hayo kwenye mabara mengine, hatua inayokwamisha juhudi za nchi hizo kukabiliana na changamoto hizo na kukwamisha juhudi za kujikwamua kiuchumi.

Mkutano huo umehudhuriwa pia na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, ambaye pia ni Gavana mbadala wa Tanzania katika Benki ya Dunia, na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Amina Khamisi Shaaban.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live