Kiongozi wa zamani wa genge la wahalifu nchini Marekani amefunguliwa mashtaka ya mauaji ya mwanamuziki nyota Tupac Shakur, yaliyotokea mwaka 1996.
Tupac alipigwa risasi akiwa katika gari yake katika jiji la Las Vegas, akiwa na miaka 25 tu. Tukio hilo limeendelea kuvuta hisia kali za mashabiki wa muziki duniani kote hususan kugonga mwamba kwa uchunguzi kwa takriban miongo mitatu sasa, lakini kesi hii mpya inafungua ukurasa mpya wa tukio hilo.
Jana Ijumaa, baraza kuu la uchunguzi katika jimbo la Nevada limemfungulia mashtaka rasmi Duane "Keffe D" Davis, mwenye miaka 60, kwa kosa moja la mauaji kwa kutumia silaha ya moto.
Polisi katika jimbo hilo wanadai kuwa kiongozi huyo wa zamani wa genge la kihalifu alipanga shambulio hilo la risasi baada ya mpwa wake awali kupigana na Shakur ndani ya casino.
Davis alikamatwa Ijumaa asubuhi karibu na nyumani kwake na atapandishwa mahakamani ndani ya siku chache zijazo.
Greg Kading, ambaye ni kachero mstaafu wa polisi ambaye ametumia miaka kadhaa kuchunguza mauaji hayo ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa hashangazwi na kukamatwa kwa Davis.
"Watu wengine wote waliokula njama ama kushiriki moja kwa moja katika mauaji hayo wameshafariki,” Kading na kuongeza kuwa Davis ndiye mtu wa mwisho aliyesalia katika kesi hiyo.
Mwendesha mashtaka Marc DiaGiacomo amemuelezea Davis kuwa ni – kiongozi wa zamani wa gnge la kihalifu lililojulikana kama South Side Compton Crips street gang - na kazi yake ilikuwa "kamanda aliyeongoza matukio” ambaye ndiye “aliyetoa amri ya kuuawa” kwa Tupac wakati gari ya msanii huyo ilipokuwa imesimama ikisubiri taa nyekundu izime.
Katika mkutano na wanahabari, afisa wa polisi Jason Johansson amesema kushikilia kwao uchunguzi wa kesi hiyo kwa miaka yote iliyopita “hatimaye kumezaa matunda”.
Afisa huyo ameeleza kuwa mpwa wa Davis aliyefahamika Orlando Anderson (ambaye kwa sasa ni marehemu) aligombana na Tupac ndani ya casino muda mchache kabla ya rapa huyo kupigwa na risasi nne mnamo Septemba 7, 1996. Tupac alifariki siku chache baadae aikwa hospitalini..
Bwana Johansson aliwaonesha wanahabari mkanda wa video (uliorikodiwa na kamera za ulinzi za hoteli) ukionesha Anderson akipigwa, na kudai kuwa kupigwa risasi kwa Tupac ilikuwa ni kulipiza kisasi kwa shambulio la awali la Anderson.
Afisa huyo alifafanua kuwa ilibainika mapema tu kuwa tukio hilo lilikuwa lina mafungamano na magenge ya kihalifu, na kuwa kesi hiyo ilikuwa ikifanyiwa marejeo mara kwa mara. Hata hivyo iliwachukua mpaka mwaka 2018 ambapo taarifa mpya ziliibuka na kufanya kesi hiyo “kupata makali mapya”.
Bwana Johansson pia ameeleza juu ya “kukiri kwake mwenyewe” bwana Davis kwa vyombo vya Habari kuwa alikuwa ndani ya gari ambayo risasi zilirushwa.
Katika mkutano huo na wanahabari kiongozi wa polisi Sheriff Kevin McMahill alisema kwa hisia kuwa "kwa miaka 27 familia Tupac Shakur imekuwa ikisubiria haki itendeke".
"Kuna watu wengi sana ambao hawakuamini kuwa uchunguzi wa mauaji ya ulikuwa ni kitu muhimu kwa kitengo chetu cha polisi. Nipo hapa kuwaambia: hilo halikuwa ni jambo la kweli," ameeleza kiongozi huyo na kuongeza, "Lengo letu siku zote limekuwa ni kuhakikisha kuwa wale wote waliohusika na mauaji ya Tupac wanatiwa nguvuni.”
Shakur, ambaye jina lake la kisanii lilikuwa likiandikwa kama 2Pac, alitoa alabamu yake ya kwanza mwaka 1991. Na tokea hapo akendelea kutoa vibao vikali na kumfanya kuwa ni moja ya wasnii wakubwa zaidi wa hip-hop kuwahi kutokea.
Kifo chake kimeangaziwa katika filamu kadhaa ambazo zimekuwa zikijaribu kutegua kitendawili cha nani aliyehusika na nini kilichosababisha mauaji hayo.
Kwa ujumla 2pac ameuza zaidi ya nakala milioni 75 za kazi zake duniani kote. Baadhi ya vibao vyake maarufu zaidi ni California Love, All Eyez On Me na Changes.
Pia alipata umaarufu kwa ushiriki wake kwenye filamu kadhaa zikiwemo Juice, Poetic Justice, Above The Rim, Gridlock'd na Gang Related.