Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

SIL

Kiongozi wa dini aoa wake zaidi ya 20

Kiongozi Wa Dini Aoa Wake Zaidi Ya 20 Kiongozi wa dini aoa wake zaidi ya 20

Thu, 8 Dec 2022 Chanzo: Bbc

Mtu anayejiita nabii nchini Marekani alikuwa na wake zaidi ya 20, baadhi yao wakiwa chini ya miaka 18, Shirika la Ujasusi la Marekani (FBI) limesema.

Samuel Rappylee Bateman alidai kuwa ni mapenzi ya Mungu kwake kushiriki tendo la ndoa na wake zake, FBI ilisema.

Bateman, 46, alishtakiwa mwezi Septemba kwa kuharibu rekodi na kuzuia haki katika uchunguzi wa iwapo watoto walikuwa wakisafirishwa katika majimbo mbalimbali kwa ajili ya kufanya ngono.

Maelezo hayo yanatoka kwa hati ya kiapo ya FBI iliyowasilishwa Ijumaa.

Bateman alikuwa mshiriki wa zamani wa tawi la Kanisa la Fundamentalist Church of Jesus Christ of Latter-Day Saints (Kanisa la FLDS) - dhehebu lililojitenga la kanisa la Mormon - hadi alipoondoka na kuanzisha kikundi chake mwenyewe kilichogawanyika.

FBI ilisema kwamba Bateman alisaidiwa kifedha na wafuasi wa kiume ambao pia walitoa wake zao na watoto wao kuwa wake za Bateman.

Aliwaadhibu wafuasi ambao hawakumchukulia kama nabii, FBI ilisema.

Mnamo Agosti, Bateman alikamatwa alipogunduliwa akisafirisha trela na wasichana watatu wachanga wenye umri wa kati ya miaka 11 na 14. Aliweka dhamana lakini baadaye alikamatwa kwa madai ya kuharibu rekodi na kuzuia haki ikitendeke.

Mapema mwaka huu, wasichana tisa waliondolewa kutoka kwa utunzaji wa Bateman na huduma za watoto za Arizona, na kuwekwa katika nyumba za kikundi.

Mnamo Novemba, wanane kati yao walikimbia kutoka kwa nyumba za kikundi.

Mamlaka ya jimbo la Washington iliwafuatilia wakati afisa mmoja aliripotiwa kuona gari likiendeshwa na mmoja wa wake za Bateman, kulingana na hati ya kiapo.

Dereva huyo na wake wengine wawili wa Bateman wameshtakiwa kwa utekaji nyara katika kesi inayoendelea ya jinai, FBI ilisema.

Dereva huyo amesema alikua mmoja wa wake za Bateman alipokuwa na umri wa chini ya miaka 18, FBI ilisema.

Alijifungua miezi saba baada ya kutimiza miaka 18, kulingana na hati ya kiapo.

Katika mahojiano na FBI, hakuna msichana yeyote kati ya tisa waliowekwa nyumbani aliyetaja unyanyasaji wa kijinsia na Bateman, lakini katika majarida, walirejelea mwingiliano wa karibu naye, hati ya kiapo ilisema.

Kanisa la FLDS limetajwa kama kikundi cha chuki na Kituo cha Umaskini cha Sheria Kusini.

Mnamo mwaka wa 2011, kiongozi wa FLDS alihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kuwadhalilisha kingono wafuasi wawili wa umri mdogo aliowachukua kama bi harusi.

Chanzo: Bbc