Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kingalame awapa darasa washiriki shindano la utangazaji

11414 Pic+kingalame TanzaniaWeb

Sat, 11 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Waandishi wa habari wametakiwa kutumia taalamu zao katika kuchochea maendeleo na kuhamasisha amani ili kuifanya Tanzania kuendelea kuwa mfano kwa mataifa mengine duniani.

Pia, wameaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia masilahi ya Watanzania walio wengi badala ya kuegemea kwa watu wasio waadilifu na wenye kujali masilahi binafsi.

Wito huo umetolewa na Mjumbe wa Baraza la UWT Taifa, Grace Kingalame wakati akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Uandishi wa Habari Dar es Salaam (DSJ), alipokuwa jaji mkuu na mgeni rasmi kwenye shindano la utangazaji.

Kingalame, ambaye pia ni mtangazaji wa Televisheni ya Taifa (TBC), alisema taalama ya habari ni nyeti na haina budi kuendelea kuwa kioo na kichocheo cha maendeleo nchini na hilo litafanyika iwapo tu, maadili yake yatafuatwa.

Alisema, hata Rais John Magufuli amekuwa akisisitiza vyombo vya habari kuendelea kusaidia kuhamasisha maendeleo na anatambua mchango wake, na waandishi wa habari wanatakiwa kutomuangusha kwa kufanya kinyume.

“Hii taaluma yetu ni nyeti sana na imebeba mustakabali wa maisha ya vizazi vya sasa na vijavyo hivyo, hatupaswi kabisa kuleta mzaha ndani yake. Tunapaswa kulinda maadili na kila tunachofanya tuweke mbele masilahi ya Tanzania na siyo ya watu wachache wenye malengo binafsi," alisema Kingalame.

“Tumsaidie Mheshimiwa Rais John Magufuli kuisuka nchi yetu na kusukuma mbele gurudumu la maendeleo. Maendeleo ya haraka kwa ajili ya Tanzania mpya tunayoitaka tutayafikia kama Watanzania wote na vyombo vyetu vya habari tutaimba wimbo mmoja wa maendeleo. Ndiyo sababu ninazungumza hili kwa sababu hapa ni sehemu mwafaka ambako, wataalamu wa habari wanazalishwa,” alisisitiza.

Awali, wanafunzi wa DSJ walishiriki kwenye shindano la kusaka watangazaji bora kwenye vipengele mbalimbali. Miongoni mwa vipengele hivyo ni Mtangazaji Bora wa Michezo, Habari, Burudani na vipindi maalumu.

Kingalame aliyekuwa akishirikiana kwa karibu na Godwin Mawanja katika kufanya uamuzi, alimtangaza Jabir Hamis kuwa mshindi wa utangazaji habari za Michezo, Matlida Peter (burudani), Clement Robert (vipindi maalumu) na Florian Rutahiwa akaibuka kidedea kwenye utangazaji wa habari.

Chanzo: mwananchi.co.tz