Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kinachowaponza wasanii kupigwa hela miito ya simu na mawakala chaanikwa

69766 Simu+pic

Sun, 4 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Tatizo la wasanii kutofaidika na miito ya simu kupitia nyimbo zao kwenye mitandao mbalimbali ya simu chabainishwa.

Katika mkutano wa Chama cha wasanii wa muziki wa injili Tanzania (Chamuita), uliofanyika jana Jumamosi Agosti 3, 2019, mwakilishi wa mtandao wa Tigo, Nelson Joshua  maarufu kwa 'DJ Nelly' amesema kinachowaponza wasanii hao ni kutaka kutanguliziwa fedha wakati wa kuingia mkataba na mawakala.

Akifafanua hilo, DJ Nelly amesema utakuta msanii anataka atanguliziwe fedha yote kabla hajajua namna gani wimbo wake utazalisha hela utakapotumiwa kwenye miito hiyo ya simu hapo baadaye.

“Wakati wa kuingia mkataba, msanii anataka atanguliziwe Sh3 milioni kwa kisingizio anataka  akatengeneze video ya muziki, lakini baadaye wimbo unafanya vizuri kwenye miito na kuzalisha fedha nyingi zaidi ya hiyo aliyopewa ambayo yote wakala anaichukua.

“Pia kwa mawakala wakati mwingine wamekuwa wakiwadanganya wasanii kwamba mitandao ya simu haijawalipa wakati sio kweli wanakuwa wamechukua fedha hizo na kufanyia mambo yao, huku wakimuacha msanii akiishi kimasikini,” amesema mwakilishi huyo wa Tigo.

Hilo la mawakala, DJ Nelly amesema limesababisha kuendelea kwa majadiliano hadi sasa ya mgao wa asilimia 60 kwa 40 katika kile kinachopatikana katika miito hiyo.

Pia Soma

Amesema kwa walioingia mkataba na mawakala, walipwe moja kwa moja na mitandao au ipitie kwa wakala kwa kuwa wengine ndiyo kama hivyo wameshatanguliziwa hela.

Kwa upande wake Rais wa Chamuita, Ado Novemba amesema kutokana na kukua kwa teknolojia, wasanii wa Injili nao wanapaswa kubadilika ndiyo maana wamewaita wataalamu mbalimbali wa masuala hayo kutoa elimu kwa wasanii wakiwemo wa miito ya simu na YouTube.

Baadhi ya wasanii akiwamo David Masaga, amesema ipo haja ya mitandao ya simu kukutana na wasanii mara kwa mara kuwaelekeza namna ya kuingia mikataba ya miito hiyo.

Wakati Stella Joel, amesema mitandao hiyo inapaswa kuchukua na nyimbo za wasanii wachanga kwa kuwa ni moja ya njia ya kuwatangaza huku akieleza ana ushahidi wa baadhi ya wasanii waliojulikana kupitia miito ya simu.

Katika hatua nyingine, chama hicho kimejaza nafasi za uongozi wa Makamu wa Rais, Gwenisaga Nyanda kachaguliwa kuwa Makamu.

Wakati ile ya Katibu Mkuu imeenda kwa Lucy Wilson huku Katibu Mwenezi  akiwa Stela Joel na Mlezi wa chama akiteuliwa Mchungaji Flora Kaguo.

Chanzo: mwananchi.co.tz