Mwaka 2024 ukiwa unaelekea kuisha umeendelea kuacha majonzi kwa baadhi ya mashabiki wa kiwanda cha burudani, ikiwa ni mwezi mmoja tangu Mwigizaji Hadija Shaibu apoteze maisha, kiwanda hicho kimekumbwa na msiba mwingine baada ya mwigizaji wa filamu nchini Grace Mapunda maarufu ‘Tesa’ kupoteza maisha Novemba 2, wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwananchi Msemaji wa familia ambaye pia ni mzalishaji wa tamthilia ya Huba, Aziz Mohamed amesema Grace amepoteza maisha kwa maradhi ya Nimonia
"Kama wiki alikuwa akiumwa na kifua kidogo juzi akazidiwa, juzi kuingia jana hali ikawa siyo nzuri akapelekwa hospitali ya Mwananyamala, kama wiki hivi alisumbuliwa na Nimonia.
“Kwa uwezo wa mwenyezi Mungu tutampumzisha Jumatatu Novemba 4, saa 10 katika makaburi ya Kinondoni.
"Kesho mwili wake utaletwa nyumbani, ibada ndogo zitafanyika hapa kesho kutwa siku ya Jumatatu mwili utatoka nyumbani kuelekea viwanja vya leaders ambapo viongozi na watu mbalimbali watakuja kumuaga kutoka saa nne mpaka saa tisa na baada ya hapo tutaelekea makaburi ya kinondoni kwenda kumsitiri,"amesema Aziz
Hata hivyo Azizi amesema tasnia ya filamu imempoteza mtu mweledi anayependa watu, mcheshi mwenye nidhamu mshauri, mama na rafiki. Amesema wasanii chipukizi ni vyema kujifunza wakiwa mastaa wasiwe limbukeni kwani Tesa alikuwa msanii mkubwa nchini lakini alishirikiana na kila mtu badala ya kuishi ustaa aliokuwa nao.
Kutokana na msiba huo wasanii mbalimbali wamaigizo wamejitokeza nyumbani kwa marehemu Tesa, Sinza Vatican wakiwemo Hashim Kambi, Lamata, Aunt Ezekiel, Jacob Steven ‘JB’, Bi Mwenda na wengineo.
Akimzungumzia Tesa, JB alisema atamkumbuka Grace kwa ucheshi na utendaji kazi wake.
"Katika waigizaji wa kike Grace alikuwa ni kati ya waigizaji wazuri na wakubwa sana, mcheshi, mara ya mwisho nilimuona jana hospitali, hatukuweza kuzungumza alikuwa kwenye ICU, "amesema JB
Naye mwigizaji mwenzie Bi Mwenda amesema atamkumbuka Tesa kama mtu mcheshi, mchapakazi pamoja na kutokuwa na kinyongo na mtu.
“Alikiwa ni mchapakazi na alikuwa hachoki na kazi kama umepangwa naye kufanya kazi atakupa moyo mpaka mmalize kazi, na hata kama ukimkosea hana kinyongo utamkosea ataelewa kwa ataongea na wewe vipi ili mkae sawa, huwezi kumkuta Tesa amenuna saa zote anacheka”, amesema Bi Mwenda
Aidha mwigizaji wa Huba Mrisho Zimbwe 'Roy' ambaye alikuwa akiigiza kama mume wa Tesa amesema hatoacha kumkumbuka kwani alikuwa mtu mcheshi na mama kwa waigizaji wenzake.
“Taarifa za msiba nilizipata nikiwa nyumbani lakini jana nilikwenda kumuangalia hospitali, alikuwa mzima wa afya tu hakuwa na shida yoyote amepata tu kama nimonia kwa sababu ya hali ya hewa siku mbili tatu hizi”
“Mimi nilijifunza mengi kupitia yeye kwa sababu mimi na yeye ni kama vile familia kwangu mimi alikuwa kama mama japo alicheka kama mke wangu, alikuwa ni mtu ambaye anaweza kunishauri na nikamshauri tukakaa tukapanga tukafanya kazi zetu vizuri kwa hiyo nitamkumbuka kwa mengi mpaka sijui nimuelezee vipi”, amesema Roy
Mbali na hayo amesema Grace nje ya uigizaji wake ni mama anayeweza kupokea ushauri wa mtu yeyote. Huku maisha yake ya uigizaji yakiwa tofauti na yale ya uhalisia . Hata hivyo ameshauri waigizaji chipukizi ambao wanataka kufuata nyayo za Tesa kwa kuwataka kuwa na nidhamu, kupenda kazi zao na kuwa na maadili.
Kwa upande wa mwigizaji wa vichekesho Pascalia Silanda ‘Black Pass’ amesema kiwanda cha filamu kimepata pengo kubwa kwa sababu waigizaji kinamama ni wachache.
“Tumepata pengo kubwa kwenye tasnia ya filamu kwa sababu yeye ni mama na wamama sasa hivi kwenye tasnia ni wachache mbali ya kuwa yeye ni mama ni mwigizaji mzuri pia ni bora wa kike alifanya vizuri sana kipindi cha uhai wake kwenye tasnia amefanya filamu nyingi sana zenye kuelemisha na kuwagusa haswa wanawake,” amesema