Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

SIL

Kilichojificha ndoa za 'babu na mjukuu'

Sheikh Alhad Mussa Salum https://ippmedia.com/sw/habari/kilichojificha-ndoa-za-babu-na-mjukuu

Sun, 29 Aug 2021 Chanzo: ippmedia.com

KILA siku watu wanaoana na neno ndoa linabaki palepale katika msamiati endelevu, wenza wa jinsia tofauti wenye umri unaoendana wanaingia kwenye ubia wa maisha kimila, imani na kisheria, kiunganishi kikuu hapo ni mapenzi.

Hata hivyo, wataalamu wa walezi na ubia huo wanaenda mbali kwamba mapenzi ni kipengele tu na kuna mazito katika tafsiri 'maisha'.Hapo katika tafsiri kuu 'maisha' ndiyo leo hii kumeingia utata wa babu kumpata mwenza ambaye ni mjukuu, wenyewe wakiwabatiza jina la 'baby'.

Bibi pia hayuko nyuma na 'shallo balo', mhitimu wa sekondari miaka michache iliyoisha anasaka ajira akitokea kwa mama na baba.

Mara zote katika maisha hayo muoaji, mtoa uamuzi, mmiliki uchumi na pekee anayefaidi na mwoga kupindukia wa penzi hilo ni ama babu au bibi huyo. Je, nini tatizo katika sosholojia hii ya ndoa? Mkazi wa Sinza wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Amina Chibule, anasema uhusiano wa aina hiyo unachagizwa na kile anachokiita tamaa ya vijana kuishi maisha mazuri bila kujali madhara ya kiafya."Inasikitisha hawa mabinti wadogo sasa wanaongoza kuvunja ndoa za watu maana wanaparamia waume za watu na wazee huko mitaani.

"Yaani hawafikirii kabisa kwamba 'huyu baba kwa umri wake lazima atakuwa na familia’ na pia wanaona kama fasheni kwa kuwa baba hao ndio wanawapa jeuri ya fedha. Kama mzazi, sifurahishwi kabisa na jambo hili," analalamika.Hamis Shaaban (57), mkazi mwingine wa Sinza anashauri nchi iwe na sheria ya kudhibiti uhusiano wa aina hiyo baina ya watu wazima na vijana wenye umri mdogo.

"Kwa kweli hili suala ni la kusikitisha. Ninafikiri wengi wanaofanya haya mambo akili zao haziko sawa. Hivi unawezaje kujihusisha kimapenzi na binti mdogo ambaye kiumri ni sawa na mjukuu wako? "Haiingii akilini kabisa. Ningeshauri serikali, ninafikiri kwa sasa hatuna sheria, tuweke sheria kali dhidi ya mzee yeyote atakayejihusisha kimapenzi na binti au kijana mdogo," anashauri.

Natalia Mpalanga (22), mkazi wa Riverside wilayani Ubungo mkoani Dar es Salaam, anasema anajisikia vibaya kuona vijana wenzake wanatenda kile anachokiita kukurupukia maisha wakiamini kuwa na uhusiano wa kimapenzi na watu wazima watakuwa na uhakika wa kutunzwa na kutimiziwa mahitaji yao yote.

"Vijana wengi wana tamaa ya vitu vizuri, mafanikio yanahitaji kuwa na subira, tunapaswa kuweka juhudi katika masomo na kujishughulisha na ujasiriamali," anasema.USTAWI WA JAMIIWataalamu wa masuala ya ustawi wa jamii wanasema ndoa za babu au bibi na mjukuu zinasababishwa na mambo mengi ikiwamo umasikini, tamaa, mikumbo na maumivu ya uhusiano wa kimapenzi uliopita.

Mhadhiri Msaidizi katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii mkoani Dar es Salaam, Catherine Banda, anainyoshea kidole kadhia hiyo, akifafanua:"Mzee kuoa au kuwa na uhusiano wa kimapenzi na binti mwenye umri mdogo inaweza ikawa imesababishwa na baba mtu mzima kupoteza mwenza wake akiwa uzeeni.

"Katika mazingira hayo, hali ya upweke inamfanya atafute binti mdogo wa kuishi naye ili kumsaidia zile intimate needs (mahitaji ya ndani). Wengi wanahofu kuchukua watu wazima wenzao kwa kuwa wote wanakua hawana nguvu."Hii inamfanya mzee kwenda kutafuta binti mwenye umri mdogo, lakini msingi wa uhusiano wao unakuwa sio sahihi kabisa.

"Pia kuna tatizo la mabinti kuwa na uhusiano na mtu mzima ili kukidhi mahitaji ya kiuchumi. Hii inatokana na imani kuwa watu wazima wana kipato kikubwa, hivyo kurahisisha maisha na binti huyo kutatua shida zake kwa haraka.

"Wapo mabinti ambao ni wanafunzi wa vyuo wanatoka kimapenzi na watu wazima ili wasaidiwe kifedha hata kama wanafunzi hao wanapata sapoti kubwa kutoka kwa familia zao, jambo hili sio jema"Vijana wengi wanataka mambo makubwa  ilhali hawana uwezo kifedha. Wanataka wawe na magari na simu za bei kubwa.

Hizi tamaa zao ndizo zinawaponza hadi wanaingia kwenye uhusiano wa namna hii," Catherine anaonya.Mtaalamu huyo wa ustawi wa jamii anabainisha kuwa vijana wa kiume wamekuwa wakitumbukia katika uhusiano wa kimapenzi na mama au bibi zao kutokana na uvivu wa kufanya kazi, hivyo wanakubali kwenda kulelewa.

"Kwa ujumla, suala hili sio sawa kwa ustawi wa jamii kwa sababu linakiuka taratibu za kiutamaduni. Mapendekezo yangu ni kwamba elimu ya uhusiano lazima itolewe kwa vijana ili wafanye uamuzi sahihi juu ya nani anastahili kuwa naye kwenye uhusiano wa kimapenzi," anashauri.

VIONGOZI WA DINI

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi Inayoshughulika na Masuala ya Ndoa, Familia na Malezi Tanzania (TaMCare), Dk. Enock Mlyuka, anakosoa ndoa za babu na mjukuu, akisisitiza kuwa ndoa ni kitovu cha familia na malezi.

Dk. Mlyuka ambaye pia ni Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), anasema kinachochangia vijana kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na watu wazima au binti kuolewa na mtu mwenye umri mkubwa, ni makuzi ya vijana hao wanayotoka nayo kwenye familia zao.

"Hawa wameanza kuharibiwa kuanzia kwenye familia zao, mambo wanayofanya wameona wanakotoka, hawakuwekewa misingi bora ya kujitambua, nidhamu na maadili. Wakifikia utu uzima wanaingia kwenye uhusiano wakiwa hawajitambui sawasawa," anahadharisha.

Anataja jambo lingine ni anachokiita ulimbukeni binafsi, akifafanua kuwa kijana akikosa ajira, anakuwa na visingizio vya hali ngumu ya maisha na kuona heri alelewe na mtu mzima.

"Kitendo hicho kinamwondolea umakini wa kufanya uamuzi sahihi, anachokiangalia ni kutatua tatizo lililopo mbele yake, analelewa bila kujua mwanaume unapooa halafu ushindwe kutimiza majukumu yako, thamani inashuka, wengi wamejikuta badala ya kutatua tatizo, yanaongezeka mengine," anaonya.

Anataja sababu ya tatu ni kukosa maarifa, hivyo kijana kuingia katika taasisi ya ndoa bila kuielewa madai, misingi, kanuni na miiko yake.

"Wapo walioingia kishabiki wakidhani ndoa ni fedha wakati huo sio msingi wake. Tatizo lingine kubwa ni vijana kutokuwa na uhusiano mzuri na Mungu. Wana elimu ya utandawazi ambao unawaendesha katika ndoa zao.

"Haipiti siku sijapata simu au mtu amekuja ana mgogoro na mwenza wake. Nyingi unakuta mwanamke ni mkubwa kuliko kijana au wamepishana kidogo umri au umri unaofanana na nyingine unakuta wote ni watu wazima," anabainisha.

Nipashe Jumapili inatua mezani kwa Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, ambaye ana ufafanuzi kwamba sio kosa kijana kuoa mtu mzima au kuolewa na mtu aliyemzidi umri, lakini shida iko kwenye utu uzima wenyewe.

"Kuna utu uzima sana na utoto sana, kiutu na heshima haipendezi. Japokuwa dini haikatazi, lakini kuna vitu vya murua na heshima. Wakioana umri unaofanana au umri uliopishana kidogo, kunakuwa na heshima," anashauri.

Kiongozi huyo wa kiroho anasema vijana wa kike na kiume wanakimbilia kulelewa, wakiamini watu wazima wana fedha, hivyo kuwa na uhakika wa kuhudumiwa.

Anaonya kuwa ndoa nyingi za aina hiyo huwa hazidumu kwa sababu vijana hao baadae hukutana na wenye umri unaoendana nao na kusababisha migogoro.

*Imeandaliwa na Haika Christopher (SJMC), Leyla Joho (TUDARCo) na Sechellah Nakamba (SJMC). Taarifa za ziada: Romana Mallya.

Chanzo: ippmedia.com