Wakati ufaulu wa somo la Kiingereza katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka 2022 yakishuka, albamu, EP za wasanii kwa mwaka huu zimetawaliwa na lugha ya Kiingereza.
Katika matokeo ya mtihani wa Taifa yaliyotangazwa juzi na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) asilimia 67.71 ya watahiniwa wote katika mtihani huo walipata daraja D katika somo la Kiingereza.
Kwa mwaka huu ulioshuhudia kuwapo kwa utitiri wa albamu na EP zenye majina ya lugha ya Kiingereza, licha ya asilimia zaidi ya 95 ya nyimbo zake kutumia lugha ya Kiswahili.
Kwa sasa ni vigumu kusikia albamu zenye majina kama Ugali (Juma Nature), Binti (Lady Jaydee), Itikadi (Sugu), Ulimwengu Ndio Mama (Jay Moe), Machozi Jasho na Damu (Profesa Jay), Si Uliniambia (MB Dogg), Ng’e (Ngwair) na Kazi Yake Mola (Madee).
Inaelezwa kiu ya wasanii wa sasa kutaka kulishika soko la kimataifa kwa lengo la kupata fedha za mauzo mtandaoni ndiko kumepelekea wengi wao kupenda kuzipa albamu na EP zao majina ya Kiingereza.
Mathalani mwaka jana pekee albamu na EP zaidi ya 10 za wasanii wakubwa Bongo zilitoka kwa mfumo huo, miongoni mwa hizo ni; Sound From Africa - Rayvanny, Only One King - Alikiba, Taste - Nandy, Defination of Love - Mbosso, The Capricorn - Izzo Bizness, Promise - LavaLava, Experience - Stereo, na High School - Harmonize.
Kwa mwaka 2022 ambao unaelekea ukiongoni mambo yameendelea kuwa yaleyale, wasanii wamekipa kisogo Kiswahili katika majina ya albamu na EP zao, licha ya utunzi wa nyimbo zao nyingi kutumia lugha hiyo. Hawa ni baadhi ya waliofanya hivyo kwa mwaka 2022 pekee.
1. First of All (FOA) - Diamond Platnumz
EP hii ni mwendelezo kwa Diamond kutumia Kiingereza baada ya albamu yake ‘A Boy From Tandale’ ya mwaka 2018, hata hivyo, albamu zake mbili za mwanzo; Kamwambie (2010) na Lala Salama (2012) alizipa majina ya Kiswahili.
2. Maturity - Nandy
Hii ni EP ya pili kwa Nandy kutumia jina la Kiingereza baada ya ile iitwayo ‘Taste’ iliyotoka mwaka jana, na hata albamu yake ya kwanza, ‘The African Princess’ alipita mule mule tu.
3. Made for Us - Harmonize
Ni albamu yake ya tatu kuipa jina la Kiingereza, alianza na; Afro East (2020), High School (2021) kisha Made for Us (2022) ambayo Harmonize amedai huenda ikawa albamu yake ya mwisho kutumia Kiswahili upande wa utunzi.
4. First Born - Beka Flavour
Aliamua kuipa albamu yake hii ya kwanza jina hilo (First Born) kwa heshima ya mtoto wake wa kwanza wa kiume, Aaryan aliyejaliwa na mrembo Happiness Reuter.
5. Dedication - Ommy Dimpoz
Ni albamu yake ya kwanza tangu ameanza muziki, Dimpoz amedai jina hilo ni kama shukrani kwa mashabiki wake kwa kuwa naye kwa miaka zaidi ya 10 bila yeye kutoa albamu, ila bado waliendelea kuwa naye.
6. The King of New School - Ibraah
Baada ya kusaniwa tu Konde Music miaka miwili iliyopita, aliachia EP yake, ‘Steps’ na mwaka 2022 kaachia albamu yake, ‘The King of New School’ ambayo anadai jina hilo kapewa na mashabiki wake.
7. Flowers II - Rayvanny
Hili ni toleo la pili la EP yake Flowers, lilitoka Februari mwaka huu, ikiwa ni EP yake ya tatu baada ya kuachia New Chui (2021) na albamu, Sound From Africa (2021).
8. Love Sound Different - Barnaba
Hii ni albamu yake ya tatu kufanya hivyo, alianza na; Gold (2018), Refresh Mind (2020) na sasa Love Sound Different (2022) ambayo inatajwa na wengi kuwa albamu bora zaidi kwa mwaka huu kutokana na kushirikisha wasanii wengi wakubwa Bongo kwa sasa.
9. Goddest - Rosa Ree
Ni albamu yake ya kwanza tangu ametoa kimuziki chini ya The Industry, ameipa jina hilo kuonyesha ukubwa wa muziki wake na jina lake kama msanii wa kike ndani ya tasnia.
10. King of Heart - Jux
Hii ni albamu ya pili kwa Jux baada ya kuachia The Love Album (2019) inayotajwa kuwa bora zaidi, utunzi wake mzuri wa nyimbo za mapenzi ambazo kwa kiasi kikubwa huwashika warembo ndipo kumepelekea kuja na ‘King of Heart’.
Ukiachana na hizo kuna; The Green Light (Killy), Cinema (Maua Sama), Flight Mode (Salmin Swaggz), Endless Love (Cheed), Love Life (Mansu-Li), Romantic (Kusah) na Super Nyota - Young Killer, hii imechanganya.
Albamu na EP chache zilizotoka mwaka huu zenye majina ya Kiswahili ni; Fundi - Rich Mavoko, Rais wa Kitaa - Nay wa Mitego, Bado - Songa, Simu na Matukio - P Mawenge na Mhadhiri - Maalim Nash (Nash MC).
Wasanii wafunguka
Mwimbaji Beka Flavour amesema kama albamu imetumia lugha moja tu ya Kiswahili halafu ikapewa jina la Kiingereza, hapo anadhani kuna shinda, ila kama ndani ina mchanganyiko, ikipewa jina la Kiingereza ni sawa na ndicho alichofanya kwenye albamu yake, First Born.
“Albamu nyingi za zamani kwa mfano ukizungumzia hiyo ‘Ugali’ ya Juma Nature, albamu nzima huwezi kukutana na neno hata moja la Kiingereza au unakakuta moja au mawili. Sasa hivi muziki umekua zaidi na unasikilizwa mbali tofauti na albamu za kaka zetu zilikuwa zinasikilizwa hapa Tanzania, nimevuka sana labda Kenya,” amesema.
Watu wengine wanaotusikiliza huko hawaelewi kabisa Kiswahili, lakini wakikutana na wimbo mmoja ambao umechanganya lugha, kidogo wanaweza kupata burudani. Muziki tunataka ufike mbali ndio maana unaona tunaunga maneno ya Kiingereza kwenye nyimbo zetu hata wale wasioelewa Kiswahili waweze kusikiliza, kwa hiyo naona ni sawa,” amesema Beka.
Beka amedai kuendelea kuimba tu Kiswahili kumechelewesha sana wasanii wa Tanzania kufanikiwa kimataifa kama wenzao Nigeria na hata wasanii wa hapa wanapojaribu kuimba lugha hiyo bado kuna namna wanakosea.
“Kitu ambacho kinatushelewesha kufanikiwa kimataifa ni lugha, unaweza kuimba wimbo mzuri sana lakini ni wa Kiswahili, kwa hiyo wa mataifa mengine wa mbali hawawezi kukuelewa licha ya kupenda muziki,” amesema.
“Na hata kama tukijitahidi kuimba kwa Kiingereza bado kimekuwa hakinyooki, lafudhi yetu bado sana, tunalazimisha tunafanya vitu vya ajabu, tukiimba Kiingereza ndio tunaharibu kabisa ladha ya muziki, tofauti na ukimsikia Mnigeria kaimba Kiingereza, kwa hiyo tunaunga unga kutafuta soko lakini bado,” amesema Beka Flavaour.
Ibraah kutokea Konde Music amesema aliamua kuipa albamu yake jina la The King of New School kwa kuwa wakati anatoka kimuziki alipitia changamoto nyingi na kuweza kuzishinda, ndipo mashabiki wake wakampa jina hilo. “Nakumbuka kipindi natoka nilipitia majanga mengi wakati bado mchanga kwenye muziki, nilifanikiwa kupambana na hizo changamoto ndio mashabiki zangu wakaniita The King of New School, ndio nikaona nilitumie kwenye albamu yangu ya kwanza,” amesema Ibraah.
Kwa upande wa Juma Nature amesema bado ni mapema kwake kujua wasanii wa sasa wanataka nini kwa kufanya hivyo ila anahisi sababu kubwa ni kutaka kufanya vizuri katika soko la kimataifa. “Siwezi kujua watu wanafikia nini maana kila msanii ana malengo yake ila Kiingereza ni lugha nayo pia, kama umelenga soko la kimataifa ina maana unakuja na mkakati wa kufanikiwa, nahisi wanapoandia Kiingereza wanalenga soko la Kimataifa,” anasema Juma Nature.
Utakumbuka hadi sasa Juma Nature ametoa albamu tano ambazo zote zimebeba majina ya lugha ya Kiswahili, albamu hizo ni kama; Nini Chanzo (2001), Ugali (2003), Ubinadamu Kazi (2005), Zote Historia (2006) na Tugawane Umaskini (2009).