Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiba Sio Mtu Kabisa, Alaza Watu na Viatu

Alikiba Utu Video Kiba Sio Mtu Kabisa, Alaza Watu na Viatu

Thu, 3 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MFALME wa Bongo Fleva, King Kiba anadaiwa kuwalaza na viatu mahasimu wa kimuziki baada ya kufanya maajabu makubwa.

Achana na yale mamilioni aliyozoa kupitia Serikali ya Tanzania chini ya mwavuli wa Chama cha Haki Miliki (COSOTA) katika ugawaji wa mirabaha, lakini jamaa amegusa wengi kupitia wimbo wake unatamba zaidi kwa sasa wa Utu.

Kwenye viwanja vingi mno vya burudani wikiendi iliyopita, wimbo huo uligeuka Wimbo wa Taifa kwa namna ulivyokuwa unapigwa kwa kurudiwarudiwa huku mashabiki wakiuimba mwanzo hadi mwisho.

“Na umebarikiwa utu na utulivu. Umebarikiwa utu na utulivu. Licha ya upole na uzuri. Una utu na utulivu. Umebarikiwa utu na utulivu…” zilisikika shangwe kwenye viwanja vya burudani watu wakiitikia korasi ya Wimbo wa Utu kutoka kwa King Kiba.

Baadhi ya mashabiki waliozungumza na gazeti hili walikuwa na maoni tofauti, lakini yote kwa yote walinyoosha mikono juu kumkubali King Kiba;

“Kuna nyakati tuwe wakweli, Utu ni wimbo bora wa karne hii au katika historia ya Bongo Fleva.”

“Ubora wa Utu upo kwenye mashairi bora na utunzi wenye staha na kuheshimu malezi ya Kitanzania.”

“Pia video yake ni bora mno, ina mazingira bora ya kutazama utalii Mlima Kilimanjaro na Ziwa Duluti, Arusha na kuitangaza nchi.”

“Ni marufuku kulinganisha Utu na nyimbo zenye wasikilizaji wengi wa mchongo.”

Hiyo ni sehemu ya maoni ya mashabiki mbalimbali wa muziki nchini Tanzania.

King Kiba ameachia video ya wimbo huo wa UTU ambao ni wimbo wa 14 kwenye album yake ya Only One King aliyoiachia mwishoni mwa mwaka jana.

Kupitia ujumbe aliochapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram, Kiba anasema kwamba wimbo huo ni zawadi kwa mashabiki wake ambao wamesapoti kipaji chake kwa muda mrefu sasa.

“Utu (official video) is out now on YouTube. Go check it now. This is the best gift to my fans, enjoy!” Aliandika Kiba.

Wimbo wa Utu unaonekana kupendwa zaidi na mashabiki wake kutokana na maudhui yake ya mwanaume ambaye anaahidi kujitoa mhanga kumpenda mpenzi wake daima.

Huu unatajwa kuwa wimbo bora utakaosikilizwa zaidi kuelekea msimu huu wa Valentine’s Dar (Februari 14) na ndiyo maana Kiba amezichanga karata zake vizuri bila kelele na sasa anakwenda kulikamata soko hilo la Wapendanao.

Tayari video ya wimbo huo imeweka rekodi ya kushika namba moja kwenye YouTube za kuziondoa videop za wasanii kama Diamond, Harmonize na wengine wote na sasa yeye ndiye anatawala.

Mbali na Wimbo wa Utu, Kiba ameendelea kutamba kwani albam yake ya Only One King ndiyo albam pekee Afrika Mashariki kwenye orodha ya albam kumi zilizofanya vizuri barani Afrika.

Hadi sasa albamu hiyo imeweka rekodi za kila aina kwenye majukwaa mbalimbali ya usikiliza muziki ikiwemo Boomplay, Deezer, Spotify, YouTube na Apple Music.

Mbali na Watanzania, Tommy Flavour, K2ga na Abdu Kiba wa Kings Music, King Kiba aliwashirikisha wasanii 8 wakali barani Afrika hivyo kuifanya kusikilizwa kwenye nchi ambazo kuna washiriki wake.

Kwenye albam hiyo, Kiba ameimba na Rudeboy, Mayorkun na Patoranking kutoka Nigeria, Sarkodie (Ghana), Nyashiski, Khaligraph Jones na Sauti Sol (Kenya) pamoja na Blaq Diamond, nguli wa miondoko ya Afro Pop kutoka Afrika Kusini.

Kiba ni miongoni mwa wasanii ambao wamepeperusha bendera ya Tanzania kwa muda mrefu akiwa sehemu ya wasanii wachache ambao hawatumii kiki kusukuma muziki wao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live