Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiba; Nguli wa Bongo Fleva anayeishi dunia yake

Kiba Wazi Kiba; Nguli wa Bongo Fleva anayeishi dunia yake

Thu, 23 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Unapotaja miamba ya muziki wa bongofl eva huwezi kulikosa jina la Ali ‘Kiba’ Saleh, mkurugenzi wa lebo ya Kings Music ambaye amekuwa kioo kwa wasanii wengi chipukizi.

Ali Kiba ambaye alianza kuimba muziki mwaka 2004, katika kipindi cha miaka 19 aliyodumu kwenye muziki amefanikiwa kuachia albamu tatu ambazo ni Cinderella,(2008), Ali K4 Real (2009) na Only One King (2021).

Albamu ya Cinderella aliyoiachia mwaka 2008 iliweka rekodi ya mauzo kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki. Kiba aliweka rekodi ya kuwa msanii wa kwanza kutoka nchini kufanya kazi na mkongwe wa Rnb duniani, Robert Kerry ‘R Kerry’ kwenye wimbo wa ONE8 – Hands Across the World ulioachiwa mwaka 2010.

Kiba pia amefanyakazi akiwa na wakali wengine kama Fally Ipupa (DRC), Face Idibia (Nigeria), Amani (Kenya), Movaizhaleine (Gabon), 4X4 (Ghana), Navio (Uganda) na JK (Zambia).

Aliwahi kukaa miaka mitatu bila kuachia kazi yoyote tangu mwaka 2012 hadi mwaka 2015 aliporudi na kuachia nyimbo mbili ‘Mwana’ na ‘Chekecha’ ambapo alifanikiwa kutwaa tuzo sita.

Mwaka 2015 msanii huyo aliweka rekodi ya nyimbo zake kupakuliwa mara nyingi zaidi kuliko msanii mwingine na kujipambanua kuwa moja ya wasanii wakubwa hapa nchini, Afrika na duniani kwa ujumla.

Kiba aliendelea kuwa na muendelezo mzuri mwaka 2022 baada ya kutwaa tuzo tano kwenye Tanzania Music Awards ambapo alitwaa kwenye kipengele cha Albamu bora ya mwaka ambayo ni Only one King, Msanii bora wa kiume ,Video bora ya mwaka katika wimbo wa ‘Salute’ aliomshirikisha Rudeboy,Mwandishi bora wa mashairi na Msanii bora wa Afrika Mashariki.

Kiba ni maana halisi ya talanta Katika kipindi cha miaka 19 ambacho yuko kwenye muziki wa bongofleva, Kiba ameendelea kuwa gumzo kila anapoachia kazi zake kutokana na ubora wake wa kuandika mashairi.

Ndani ya miongo miwili kwenye kiwanda cha bongofleva, Kiba ndio msanii ambaye amehusika katika matukio mengi zaidi ya kijamii kuliko msanii yoyote wa muziki hapa nchini kwa kujaribu fursa zaidi ya moja na kufanikiwa kwa ubora ule ule kama ilivyo kwenye muziki.

Ukiachana na kufanya vizuri kwenye muziki Kiba ni miongoni mwa watu wenye uwezo mkubwa wa kusakata kabumbu ambapo mwaka 2018 alijiunga na Coastal Union ya Tanga ambako alidumu kwa msimu mmoja na kuachana na Wagosi wa Kaya.

Mbali na Coastal Union, Kiba amekuwa akiingoza timu ya Tabata All Stars kwenye mashindano ya Ndondo Cup ambayo yamekuwa yakiandaliwa kila mwaka na kampuni ya Clouds Media.

Licha ya kuwa kwenye muziki kwa muda mrefu Kiba ameendelea kuwa na nidhamu ile ile jambo linalofanya asichuje huku lebo yake ya Kings Music ikiwa mfano kwa kuibua vijana wapya wenye vipaji vizuri vya kuimba.

Kupitia lebo yake ya Kings Music , ambayo yeye ni Mkurugenzi imeibua wasanii kama Ki2ga, Cheed , Killy , Vannilla na Killy Paul ambavyo ni baadhi ya vipaji ambavyo hakuna aliyekuwa akifikiri wanaweza kutengeneza majina yao kupitia muziki.

Lakini pia Kings Music ni miongoni mwa lebo ambazo ni nadra kuona wasanii wakiondoka huku wakilalamika kutotendewa vyema au kunyonywa hii inaonesha wazi kuwa Kiba ni msimamizi mzuri kwa vijana wanaochipukia.

Ndio sababu ni ngumu kuona wasanii kutoka lebo ya Kings Music kukumbwa na skendo za ajabu hii inatokana na usimamizi mzuri kutoka kwa Mkurugenzi wake ambaye heshima na adabu imemfikisha hapo alipo.

Hapi amvuta kwenye Kilimo Wakati wengine wakipambana kujitafuta kwenye muziki Kiba ameamua kujiingiza kwenye kilimo baada ya kuvutiwa na kile kinachofanywa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi ambaye sasa amekuwa mfano wa kuigwa.

Kiba anasema kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram kwamba kilimo ni eneo jingine ambalo amewekeza ukiacha muziki. Anasisitiza kuwa kama unataka kupiga fedha, basi unapatikana kwenye kilimo amekiri kuwa kwenye kilimo kuna uhakika na kunaweza kubadili maisha ya vijana wengi.

Siku za karibuni watu wengi wameanza kujiingiza katika kilimo kutokana na juhudi ambazo serikali kupitia Wizara ya Kilimo imekua ikizifanya kuboresha sekta hii ambayo kipindi cha nyuma ilionekana ni ya watu wa mikoani au vijijini.

Lalala na Mahaba zaendelea kuonesha ukubwa wake Baada ya kimya cha kitambo kifupi, Kiba amekuja kivingine mwaka huu baada ya kuachia nyimbo mbili ndani ya wiki nne ambazo tayari zimekuwa zikifanya vizuri kwenye chati mbalimbali za muziki kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

Wimbo wa Mahaba ambao aliuachia wiki tatu zilizopita hadi sasa umefikisha watazamaji milioni 3.4 na kuufanya kuwa wimbo uliofuatiliwa na watu wengi kwenye Youtube chaneli yake.

Siku sita zilizopita aliachia wimbo wa Lalala ambao amewashirikisha K2ga na Abdul Kiba ikiwa ndio kwanza umeachiwa tayari wimbo huo umefikisha watazamaji milioni 1.5 na kuwa wimbo uliofuatiliwa zaidi ndani ya wiki hii.

Kiba ameendelea kutoa darasa kwa wasanii chipukizi ambao wamekuwa wakimtumia nyota huyo kama kioo ili waweze kufika daraja la juu kwenye fani hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live