Rapa wa Compton Kendrick Lamar afunguka kuhusu maisha yake ya kiroho ambapo amekiri kuwa “huongea na Mungu moja kwa moja.” Katika mahojiano aliyoyafanya hivi karibuni na SZA kupitia jarida la Harper’s Bazaar, Kendrick Lamar aliulizwa kuhusu “maisha yake ya kiroho” na jinsi anavyotumia imani yake katika shughuli zake za kila siku, K.Dot alieleza kuwa Maisha yake ya kiroho yana nafasi kubwa sana katika maisha yake, hasa mazungumzo yake na Mungu, ambapo alikiri kuwa huwa anasikia sauti ya Mungu.
“Huu sio Utani lakini, naongea na Mungu moja kwa moja. Kama vile nafikia hatua nahisi napoteza akili. Lakini Mungu hunikumbusha, ‘Hapana, ni mimi huyu.’”
Hitmaker wa “Not Like Us” aliwahi kuzungumza kuhusu mazungumzo yake na Mungu mapema mwaka huu, wakati wa sherehe za kuhitimu Chuo cha Compton, ambapo alikuwa mgeni rasmi na alieleza jinsi ilivyo muhimu kuzungumza na Mungu. Pia mwaka 2015, aliliambia jarida la Billboard kuwa yeye ni miongoni mwa wateule wa Mungu, jambo lililomsaidia kuepuka njia za uhalifu na vurugu akiwa anakua Compton.