Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Katuni zitanilipa zaidi ya ualimu ninaosomea chuoni’

18278 Pic+katuni.png TanzaniaWeb

Thu, 20 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mara nyingi moyo huwa na amani unapofanya kazi unayoipenda bila kulazimishwa wala kuchaguliwa na mwingine. Awe mzazi au mlezi.

Jambo hilo humfanya muhusika kufanya kazi yake bila manung’uniko, kujituma na kuhakikisha anafanya kila awezalo iwe bora zaidi ya jana.

Maneno haya yanajidhihirisha kwa Derick Nongwa (25), mwanafunzi wa shahada ya elimu katika Chuo Kikuu Jordan asiye na ndoto za kuajiriwa pindi atakapohitimu. Badala yake, anataka kusimamia anachokiamini na kukipenda kuimiza ndoto zake.

Nongwa ni mchoraji wa katuni kielektroniki. Anasema licha ya kukosa darasa la ana kwa ana la uchoraji katuni lakini alihakikisha ndoto hiyo inafanikiwa kwa kujifunza kupitia mtandao wa Youtube.

“Muda wangu mwingi wa mapumziko nilikuwa nautumia kuangalia video mbalimbali za wachoraji wa nje ambao tayari wanafanya vizuri na kuiga ujuzi wao hadi nilipoona nimeelewa,” anasema Nongwa.

Anasema japo ilimchukua muda mrefu kujifunza kabla ya kuanza kuchora katuni zake mwenyewe, hakuwahi kukata tamaa mpaka alipohakikisha anachokihitaji kimekamilika.

“Nilianza kuchora mwaka 2016 lakini baadae niliona ujuzi nilionao hautoshi ndipo nilitafuta wenzangu wanaofanya kazi hii ambapo tulitengeneza kundi la WhatsApp kwa ajili ya kubadilishana uzoefu,” anasema Nongwa.

Wakati anaanza kufanya kazi hiyo, anasema matumizi makubwa yalikuwa kununua kifurushi cha intaneti aweze kujifunza kwa kina kwa sababu tayari alikuwa na kompyuta.

Gharama ya kupata katuni zake, inategemea ukubwa wa picha anayotuma mteja huku baadhi zinazoletwa kama wazo ndizo huhitaji penseli na karatasi kabla mchoro halisi haujatengenezwa kielektroniki.

“Mimi nachora katuni kwa kutumia picha utakayo nitumia, kama picha ni nusu gharama yake ni Sh10,000 na mwili mzima ni Sh20,000. Ikiwa nusu ya watu wawili ni Sh25,000 na nzima ya idadi hiyo ni Sh40,000,” anasema.

Japo soko la biashara hiyo bado si kubwa sana, lakini kuna wakati anaweza kuchora hadi picha 25 kwa siku kutokana na wingi wa wateja ingawa zipo siku ambazo anaweza kuchora moja lakini ikamingizia Sh100,000.

Nongwa anasema wateja wake wengi huwapata kupitia matangazo mbalimbali katika kurasa za mitandao ya kijamii.

“Wengine inakuwa ngumu kuniamini kwakuwa hawanijui hivyo kuwa ngumu kutuma pesa niwafanyie kazi bila kuniona. Wengine wanauliza ofisi zilipo ili waje ndiyo wanipe kazi lakini mwisho wa siku huwa nawaelewesha,” anasema Nongwa.

Kutokana na uchoraji katuni anaoendele anao tangu alipoanza, anasema amenunua pikipiki mbili anazozikodisha kama bodaboda hivyo kumuongezea kipato kukidhi mahitaji yake huku akiwa na mpango wa kujitanua zaidi.

Nongwa anakusudia kumiliki ofisi kubwa ya uchoraji wa katuni na utengenezaji wa mabango ya matangazo.

“Japo natengeneza logo na mabango lakini nikipata ofisi yangu nitaweza kufanya kazi kwa uhuru tofauti na sasa ninafanyia ndani ya chumba change, inakuwa ngumu kumleta mteja,” anasema Nongwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz