Ndoa mpya ya Kanye West inatazamiwa kutoa mwelekeo mpya wa maisha yake ikiwa ni miezi michache tangu kukamilika kwa talaka yake na aliyekuwa mke wake, Kim Kardashian, kupoteza Ubilionea wake, huku akisumbuliwa na kile kinachotajwa ni matatizo ya akili.
Jumanne ya wiki hii, Februari 21, Kanye alionekana tena akiwa na mke wake mpya, Bianca Censori huko Los Angeles, Marekani tangu kuripotiwa kufunga ndoa ya faragha na yenye utata Januari 9, 2023.
Hata hivyo, wimbo wa Kanye ‘Censori Overload’ uliotoka hivi karibuni unathibitisha kufunga ndoa, moja ya mistari inasema; An the Bible said / I can’t have anymore sex / Till marriage (Na Biblia ilisema siwezi tena kufanya ngono hadi ndoa).
Kanye na Censori walikutana Novemba 2020 baada ya Censori kuhamia Los Angeles akitokea kwao Australia, Kanye alimtumia ujumbe Instagram na kumwambia aende LA kumfanyia kazi katika kampuni yake, Yeezy kama Mbunifu Mkuu.
Censori, 27, ambaye ana Shahada ya Uzamili aliyoipata Chuo Kikuu cha Melbourne, Australia, akizungumza na Hypebeast mwaka 2021 alisema tangu akiwa mtoto alivutiwa sana na shughuli za ubunifu hasa za kisanii.
Baada ya taarifa kusambaa kuwa amefunga ndoa na Kanye, ukurasa wa Instagram wa Censori uliokuwa na wafuasi 16,500 na machapisho 27 ulitoweka, huku aliyekuwa mke wa Kanye, Kim Kardashian akirusha vijembe.
“Kumbuka tu, ni kawaida kondoo mweusi kugeuka kuwa mbuzi. Endelea kupambana,” aliandika Kim katika Insta Story na kuongeza, “Watu wanaotaka kukuona ukishinda, watakusaidia kushinda. Kumbuka hilo”.
Mtandao wa Page Six unadai Kim anamchukua Censori na amekuwa akimfahamu kwa muda, licha ya Kim kuwa mrembo, amekuwa na tabia ya kuchukia wasichana warembo. Chanzo chao kilieleza.
Mwishoni mwa Desemba 2022 Kim alitokwa na machozi katika mahojiano kufuatia matamshi ya chuki ya Kanye kwa jamii ya Wayahudi, Kim alidai amekuwa akiwalinda watoto wao wasijue mambo hayo aliyofanya baba yao.
“Siku moja watoto wangu watanishukuru kwa kutomkashifu baba yao, kwa hakika nilimlinda na bado nitamlinda machoni pa watoto wangu. Kwa hiyo, nyumbani kwangu, watoto hawajui chochote kinachoendelea huko nje.” alisema Kim.
Utakumbuka Aprili 2012 ndipo uhusiano wa Kanye na Kim ulianza, walifunga ndoa Mei 2014, wamejali watoto wanne ambao ni North (2013) na Saint (2015), huku Chicago (2018) na Psalm (2019) wakilizaliwa kwa njia mbadala, yaani mwanamke mwingine alibeba ujauzito kwa niaba ya Kim.
Aprili 2015 walisafiri hadi Yerusalemu ili kubatizwa North katika Kanisa la Mtakatifu James, Kanye alifichua kuwa awali alifikiria kutoa ujauzito wa North lakini tangu wakati huo amekuwa akipinga vitendo vya utoaji mimba.
Tangu Julai 2020 Kim alianza mchakato wa kuachana na Kanye, Februari Kim aliwasilisha kesi ya talaka iliyokuja kukamilishwa Novemba 2022. Kanye aliamriwa kulipa Kim Dola200,000, wastani wa Sh467.6 milioni kila mwezi kwa ajili matunzo ya watoto.
Kanye aliwahi kuwa na mahusiano na wanawake wengine kama Alexis Phifer (2000 – 2006), Amber Rose (2008 – 2010), Julia Fox (2021), Venetria (2022) na sasa Censori.
Hadi mwaka 2021 Kanye alikuwa Bilionea akiwa na utajiri wa Dola1.8 milioni, kwa mujibu wa Forbes, Oktoba 2022 utajiri wake uliporomoka hadi Dola400 milioni na kupoteza hadhi ya Ubilionea baada ya Adidas kukatisha mkataba wao wa kibiashara kufuatia matamshi yake ya chuki.
Oktoba 2021 ombi lake na kubadilisha jina kisheria kutoka ‘Kanye Omari West’ hadi ‘Ye’ lilikubaliwa, alisema alifanya hivyo kwa sababu za kibinafsi, ila mwaka 2018 alidai ‘Ye’ ndilo neno linalotumiwa sana katika Biblia likiwa linamaanisha ‘Wewe’, kwa hiyo; mimi ni wewe, mimi ni sisi.
Amekuwa akihusishwa kuwa na matatizo ya afya ya akili kwa miaka, Novemba 2016 alikatisha matamasha yake 21 ikidaiwa ana upungufu wa maji mwilini na kukosa usingizi, ila inasemekana alipolazwa hospitalini alikuwa na mshtuko na mfadhaiko muda wote.
Kwa miaka Kanye amekuwa kutumia dawa ya kupunguza msongo wa mawazo na mfadhaiko, Lexapro, katika wimbo wake ambao haujatoka ‘I Feel Like That’ anadai kuhisi dalili nyingi za mfadhaiko na wasiwasi kila mara.
Mwaka 2016 aligunduliwa na ugonjwa wa Bipolar ingawa hilo hakuweka wazi hadi mwaka 2018 alipotoa albamu yake ‘Ye’, alimwambia Rais Donald Trump ilikuwa taarifa mbaya kwake. Katika mahojiano mwaka 2018, Kanye alisema alikuwa amezoea kutumia dawa za Opioids, pengine urahibu wa dawa hizo ndio ulimletea matatizo hayo na mara nyingi ana mawazo ya kujiua!.