Mama mzazi wa Marehemu, Steve Kanumba, Bi. Mutegoa amezungumza kwa uchungu akidai licha ya mtoto wake kuacha filamu nyingi ambazo mpaka leo zinafanya vizuri, yeye hajawahi kupata fedha yoyote kutokana na usambazaji wa filamu hizo.
Bi Mutegoa alidai kwamba Kanumba alikuwa ameuza hakimiliki zote za kazi zake, hali ambayo ilimfanya hata alipojaribu kutengeneza filamu ya kumbukumbu za Kanumba, akaambiwa hana haki ya kutumia picha za mwanawe.
“Kwa bahati mbaya, wakati Kanumba anafanya kazi zake, alikuwa anauza kila kitu, mpaka yaani na roho yake. Kwa hiyo mimi sina haki yoyote ya ile kazi ya Kanumba” akisema.
“Na kwa bahati mbaya wengine hata hofu ya Mungu hawana, kuna mmoja nilimuomba kutumia picha za Kanumba kwenye filamu ya kumbukumbu za Kanumba, hakuwa tayari kunipa ushirikiano,” alisema Bi Mutegoa.
Alisema kwamba suala hilo limekuwa likimkosesha usingizi sana na kipindi kimoja serikali ya awamu ya tatu ilimsimamia mpaka moja ya kampuni zinazosambaza kazi za filamu za Kanumba kumlipa hakimiliki kidogo, lakini kampuni nyingine hata senti tano hajapata kuiona.