Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kampuni kubwa ya muziki duniani kuondoa nyimbo zake TikTok

Kampuni Kubwa Ya Muziki Duniani Kuondoa Nyimbo Zake TikTok Kampuni kubwa ya muziki duniani kuondoa nyimbo zake TikTok

Wed, 31 Jan 2024 Chanzo: Bbc

Kampuni kubwa ya muziki duniani Universal Music inatazamiwa kuondoa mamilioni ya nyimbo zake kwenye TikTok baada ya kuvunjika kwa mazungumzo kuhusu malipo.

Hatua hiyo ingemaanisha kuwa mtandao huo wa kijamii hautaweza tena kupata nyimbo za wasanii wakiwemo Taylor Swift, The Weeknd na Drake.

Kampuni ya Universal Music ilishutumu TikTok kwa "uonevu" ikasema inataka kulipa "sehemu" ya malipo tovuti zingine za mitandao ya kijamii hufanya kwa ufikiaji wa orodha yake kubwa.

TikTok ilisema Universal ilikuwa ikiwasilisha "simulizi ya uwongo".

Kampuni za muziki hupata malipo ya mrabaha nyimbo zao zinapochezwa kwenye tovuti moja kwa moja na majukwaa ya mitandao ya kijamii.

Ingawa TikTok - ambayo inamilikiwa na kampuni ya Kichina ya ByteDance - ina watumiaji zaidi ya bilioni moja, inachukua 1% tu ya mapato yote ya Universal, ilisema.

Katika "barua ya wazi kwa jumuiya ya wasanii na watunzi wa nyimbo" Universal - ambayo inadhibiti takriban theluthi moja ya muziki duniani - ilidai kuwa "hatimaye TikTok inajaribu kujenga biashara inayotegemea muziki, bila kulipa thamani sawa kwa muziki".

Universal Music pia ilisema kuwa pamoja na kushinikiza "fidia inayofaa kwa wasanii wetu na watunzi wa nyimbo", pia ilikuwa na wasiwasi kuhusu "kuwalinda wasanii binadamu dhidi ya athari mbaya za AI, na usalama wa mtandaoni kwa watumiaji wa TikTok"

Kampuni hiyo ilisema itaacha kutoa leseni kwa TikTok mkataba wake utakapomalizika tarehe 31 Januari.

Kujibu, TikTok ilisema: "Inasikitisha na kukatisha tamaa kwamba Universal Music Group imeweka mbele uchoyo wao dhidi ya masilahi ya wasanii na watunzi wao wa nyimbo.

"Licha ya simulizi ya uwongo ya Universal, ukweli ni kwamba wamechagua kuachana na usaidizi mkubwa wa jukwaa lenye watumiaji zaidi ya bilioni ambalo hutumika kama chombo cha utangazaji bidhaa na ugunduzi bila malipo kwa talanta zao," iliongeza.

Hii ni mara ya kwanza kwa Universal Music kuchukua hatua kubwa ya kuondoa nyimbo zake kutoka kwa jukwaa la kampuni ya teknolojia.

Universal inashikilia nafasi kubwa katika tasnia ya muziki iliyorekodiwa ulimwenguni.

Chanzo: Bbc