Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kalapina; Kutoka Kikosi cha Mizinga mpaka Jeshi la Israel

Kalapinaa (32).jpeg Kalapina; Kutoka Kikosi cha Mizinga mpaka Jeshi la Israel

Mon, 1 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kama kuna wasanii Bongo waliofanya Hip Hop na kufuata misingi yake vilivyo, basi miongoni mwao ni Kalapina a.k.a Nabii Koko kutoka Kikosi cha Mizinga.

Licha ya muziki wake kuzungukwa na matukio mengi ya ubabe bado haiondoi ukweli kwamba Kalapina ni msanii bora wa Hip Hop kuwahi kutokea na anayejitoa zaidi kwenye jamii kupitia harakati zake. Huyu ndiye Kalapina;.

1. Wakati wa uzinduzi wa albamu ya Kalapina, Kufa Au Kupona (2005) uliofanyika Dar es Salaam na Arusha, ndio ilikuwa mara ya kwanza kwake na wenzake kutumbuiza na ‘live band’, kilikuwa kitu kipya hasa katika Hip Hop kipindi hicho.

2. Kalapina na Solo Thang ni ndugu kabisa, yaani ni mtu na mtoto wa shangazi lakini hawakuwahi kujua hilo hadi walipokuja kuzinguana kwenye masuala ya muziki na habari hizo kufika katika familia.

3. Inadaiwa Solo Thang alikuwa haeleweni na Hashim Dogo ambaye alikuwa sehemu ya Kikosi cha Mizinga, uhasama wao ukageuka kuwa wa kundi na ndipo Kalapina alipojikuta naye ameingizwa katika ugomvi na ndugu yake bila kujua.

4. Tukio la Kalapina kuburuzwa na gari katika video ya wimbo wake, Mstari wa Mbele (2005) ni la kweli maana alitaka kuonyesha uhalisia na ilikuwa kionjo cha filamu ambayo hadi leo haijatoka, ni video iliyoshika namba moja chati za Channel O.

5. Msanii wa Hip Hop wa kimataifa aliyemvutia Kalapina hadi kuingia katika muziki ni Tupac ambaye alivuma zaidi kupitia albamu yake ya nne, All Eyez on Me (1996), huku akiuza rekodi zaidi milioni 75 duniani kote.

6. Wimbo wa Kikosi cha Mizinga, Hip Hop Bila Madawa (2008) ulikuja baada ya Kundi la Nako 2 Nako Soldiers ambao walikuwa mahasimu wao kimuziki kwa wakati huo kuwachana katika wimbo wao, Hawatuwezi.

7. Ili kujibu mapigo Kikosi cha Mizinga wakakusanya wasanii wengine nje ya kundi lao na kutoa wimbo huo uliofanya vizuri, Nako 2 Nako walikuja kujibu kupitia wimbo wao, Mchizi Wangu Remix ambao ulishirikisha wasanii wengi wa Hip Hop Bongo.

8. Akiwa shule ya msingi Mbuyuni, Dar es Salaam, Kalapina aliwahi kufundishwa na Mke wa Rais wa Nne wa Tanzania, Mama Salma Kikwete ambaye alikuwa mwalimu kwa takribani miaka 20.

9. Wasanii wa Hip Hop Bongo waliokuja miaka ya hivi karibuni ambao Kalapina anawakubali ni Nikki Mbishi, One The Incredible, Kadigo na familia nzima ya Tamaduni Muzik, hiyo ni kwa sababu walikuja na mtindo wao wa tofauti katika Rap.

10. Mtindo maarufu wa Kalapina wa kufunika jicho moja ilikuwa ni kwa lengo la kujitofautisha na wasanii wengine na kuitengeneza chapa yake tofauti, ni mtindo aliyoiga kutoka kwa aliyekuwa kiongozi wa kijeshi wa Israel, Moshe Dayan aliyefariki Oktoba 1981.

Chanzo: Mwanaspoti