Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kabla ya Zuwena wa Diamond, kuna hawa 10 walitikisa Bongo

Diamnond Na Zuwena Kabla ya Zuwena wa Diamond, kuna hawa 10 walitikisa Bongo

Sat, 18 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wimbo mpya wa Diamond Platnumz 'Zuwena' unaonekana kupata mapokezi mazuri, mkasa wake na namna ulivyosimuliwa kwa uandishi mzuri, melodi za kuvutia na video iliyobeba uhalisia vimechangia kwa kiasi kikubwa wimbo huo kupendwa na wengi. Hata hivyo, huu sio wimbo wa kwanza Bongo wenye jina la mwanamke linaloambatana na kisa chake, zipo zilizotoka na kuvuma vilivyo na kufanya majina yao kuwa maarufu katika jamii. Miongoni mwao ni wafuatao;

1. LATIFAH - MB DOGG

Licha ya maneno kuwa mengi kuwa Latifah kuna kitu amemfanyia MB Dogg bado alimpenda, mwaka 2004 akamtolea wimbo (Latifah) unaopatikana kwenye albamu yake, Si Uliniambia yenye nyimbo 10, na huo ukawa mwanzo wa ukubwa wa jina lake.

Madee ambaye alishirikishwa katika wimbo huo aliwahi kusema 'verse' yake bora kwa muda wote ni ile aliyochana kwenye ngoma ya Latifah, na ikumbukwe Ngwea ndiye alitakiwa kuwepo kwenye wimbo huo lakini P Funk Majani akamchugua Madee.

2. SALOME - DULLY SYKES

Hakuna ubishi kuwa Salome alikosea au ilikuwa bahati mbaya kumpenda Dully Sykes, mwanaume tapeli wa mapenzi aliyemkatili vibaya hadi kupelekea kujiua, hiyo ni kwa mujibu wa wimbo huo!.

Salome ni miongoni mwa nyimbo chache Bongo zenye simulizi za kusisimua, Dully aliuweka wimbo huo katika albamu yake ya kwanza, Historia ya Kweli (2003) pamoja nyimbo nyingine zenye visa vilivyomuhusishwa na wanawake kama; Julieta na Leah.

3. SOPHIA - BEN POL

Alichohitaji Ben Pol ni kimoja tu, kumpeleka Sophia wake nyumbani kwao, Mpunguzi, Mvumi, Mazengo na Mkuhungu huko Dodoma akawaone ndugu zake wa Makole wampatie zawadi ya karanga, zabibu na uhemba.

Ni moja ya nyimbo za Ben Pol zilizovuma sana akibadilika kidogo kutoka mahadhi ya RnB aliyokuwa amezoeleka nayo, ulitoka mwaka 2005 na Sophia wake katika video alifanya vizuri, kwa ujumla walibeba uhalisia.

4. VAILETI - MATONYA

Watu walichonga sana pamoja na kuongea uzushi kuwa Matonya hatoweza kumpata Vaileti ila haikuwa hivyo, akawa nawe kwenye shida na raha hadi kumtolea ngoma yake (Vaileti) inayopatika kwenye albamu yake ya kwanza, Siamini (2006).

Hata hivyo, takribani miaka miwili mbele Matonya akazama kwenye penzi jipya na mrembo 'Anita' ingawa walipishana sana, ukisikiliza vizuri 'verse'' ya Lady Jaydee aliyeshirikishwa katika wimbo huo utaelewa mambo hayakwenda vizuri.

5. RITA - MARLAWA

Baada ya Rita kubeba ujauzito alifukuzwa kwao hivyo akaenda kuishi kwa Marlaw, alipojifungua aliitwa kwao Arusha na kuzuiliwa kurudi Iringa, kilichomuumiza Marlaw ni kwamba siku Rita anarudi alifariki akiwa ameketi ndani ya gari na kumuachia mtoto!.

Mwishoni mwa wimbo huu uliotengenezwa MJ Records na Marco Chali, Marlaw anasema ni kisa cha kweli (true story), ulifanya vizuri mwaka 2007 na uliuweka kwenye albamu yake ya kwanza, Bembeleza (2007) iliyokuwa na nyimbo 12.

6. NEILA - TUNDAMAN

Mwili, nafsi na macho vilikuwa vinatamani kumuona Neila tu, mrembo aliyemkosha vilivyo kijana wa Tip Top Connection, Tundaman hadi kumtungia wimbo huo uliotoka mwaka 2008.

Rapa Chidi Benz ambaye wakati huo alikuwa kwenye kilele cha mafaniko yake alichangia wimbo huo kuwa mkubwa sana, kipindi hiki kila msanii alitaka kufanya kolabo na Chidi na kila aliposhiri ngoma ilikuwa lazima iwe moto.

7. REGINA - AKIL THE BRAIN

Baada ya Akil The Brain kufikia tamati kuwa moyo wake umependa Regina kwa asilimia zote alimtungia wimbo akimshirisha Steve2K, ulifanya vizuri sana na ulibeba jina la albamu yake iliyotoka mwaka 2004.

Oktoba 2022 Diamond alitumia kionjo cha wimbo huo katika wimbo 'Jugni' ambao ameshirikishwa na msanii maarufu India, Diljit Dosanjh, huu ni uthibitisho kuwa Regina wa Akil The Brain hapoi wala haboi.

8. IVETA - SAJNA

Walikuwa wanapenda huko kijijini kwao ila fedha ndio ilikuwa kikwazo hadi kushindwa kuoana, hivyo Sajna akaenda mjini kutafuta maisha, akiwa huko ndipo akamtungia wimbo Iveta akimsisitiza asichoke kumngojea kwani bado anamtafutia.

Iveta ni moja ya nyimbo bora Bongo zilizotengenezwa Tetemesha Records na Kid Bwoy na ndio uliobeja jina la albamu yake ya kwanza iliyotoka mwaka 2010, na hadi sasa ukitaja waimbaji wakali waliwahi kutokea kanda ya Ziwa ni vigumu kuacha kutaja jina la Sajna.

9. ASHA - TID

Roho ya TID a.k.a Mzee Kigogo ilipitia kipindi kigumu pale alipotaka kumuoa Asha lakini hana fedha, hivyo Asha anapaswa kumuelewa anapokuwa bize maana anasaka fedha za harusi, hiyo ni kwa mujibu wa wimbo huo.

Aliwashirikisha Top Band huku mikono ya Lamar kutokea Fishcrab ikuhusika, wimbo huu ulitoka mwaka 2009 na moja nyimbo kubwa alizowahi kuzitoa TID katika maisha yake ya muziki.

10. SALOME - DIAMOND PLATNUMZ

Mwendo na shepu, vyote kwake vilikuwa mwanana kwa Salome achilia mbali akinyonga, hii ndio sababu ya kumshika Diamond hadi kumwandika wimbo huo uliotoka mwaka 2016 akimshirikisha Rayvanny.

Ikumbukwe Diamond amechukua vionjo kutoka kwenye wimbo wa Saida Karoli, Maria Salome kitu kilichofanya ngoma yake kufunika zaidi, wasanii wengine kama Darassa na Belle 9 kupitia nyimbo zao, 'Muziki' na 'Give It to Me' wamefanya hivyo pia.

Ukichana na hao, wasanii wengine Bongo waliowahi kutaja majina ya warembo na visa vyao katika nyimbo zao ni; Rama Dee (Sarah), Mac Voice (Sarah), Beka Flavour (Saraphina) na Linex (Salima) ft. Diamond Platnumz.

Chanzo: Mwanaspoti