Msanii maarufu wa Bongo Movie, Blandina Chagula 'Johari' amesema hatapumzika kufanya sanaa kwani haina cha mkubwa na mdogo hata nafasi ya bibi atacheza kama wengi wanavyomwita.
Baada ya kurejea kutoka Nigeria alikokwenda kushiriki tuzo za Music video Africa awards kipengele cha Mwigizaji Bora wa Kike wa Mwaka na Tamthilia Bora ya Mwaka, ameliambia Mwanaspoti wengi wamekuwa wakimwona mzee na kutaka apumzike kufanya sanaa, bila kujua kazi ya uigizaji inaruhusu kila rika na hajali maneno ya wanaomwita bibi.
Johari ambaye tamthilia ya Wimbi ndiyo iliyompa tuzo moja kati ya mbili amesema hataacha kuigiza hadi mwenyewe aseme imetosha kwa sababu ni kazi anayoipenda na hata ubibi wake anataka uheshimiwe.
"Kila kukicha naitwa bibi, mara nimezeeka, yaani ili mradi tu wanataka kunivunja moyo katika kazi yangu hii ya sanaa. Sasa mimi nasema, pamoja na huu ubibi wangu, huu uzee wangu, naomba niheshimiwe sana katika sanaa, na hata kama nikiwa bibi kwani hakuna nafasi za kucheza bibi au mtu mzee? Sasa nawaambia tu, kupumzika kwenye hii sanaa ni hadi mimi mwenyewe niseme basi na siyo maneno ya watu kuniambia nipumzike," amesema.
Amesema amepata uchungu sana kupata hizo tuzo huko Nigeria hivyo, atahakikisha anapambana ili kazi zake zifanye vizuri tuzo ziendelee kuja Tanzania.
"Hizi tuzo nimezipata kwa uchungu sana. Hili ni jambo la kujivunia sana. Nitazidi kupambana ili tuzo ziendelee kuja Tanzania."