Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

SIL

Jinsi migogoro ya Ndoa inavyoliweka hatarini taifa

Ndoa  ED Jinsi migogoro ya Ndoa inavyoliweka hatarini taifa

Sun, 28 Nov 2021 Chanzo: ippmedia.com

​​​​​​​MIGOGORO ya ndoa ni janga jipya kwa ustawi wa taifa. Hali hiyo inatokana na kushamiri kwa migogoro na kuvunjika kwa ndoa huku athari zake kijamii na kiuchumi zikiwa kubwa.

Hayo yalibainika hivi karibuni katika uzinduzi wa programu maalum kwa ajili ya kuipatia ufumbuzi migogoro ya ndoa ambayo imesababisha athari mbalimbali zikiwamo kusambaratika kwa ndoa, mauaji ya wanandoa kwa sababu ya wivu wa kimapenzi, ongezeko la watoto wa mitaani na wanaolelewa na mzazi mmoja.

Katika uzinduzi wa program hiyo, maarufu kama Kliniki ya Ndoa na Uhusiano, mwishoni mwa wiki iliyopita, wadau mbalimbali walieleza ukubwa wa tatizo tofauti na inavyolichukulia.

Hali halisi inaonyesha kwamba migogoro na kuvunjika kwa ndoa vinashika kasi na hata kutishia nguvu kazi ya taifa kwa kuwa waathirika wa tatizo hilo ni watu ambao ni tegemeo katika kufanya kazi.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Ofisa mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Emmy Husdon, alisema migogoro ya ndoa imesababisha ongezeko la talaka katika taasisi hiyo, hali ambayo inaonyesha tatizo ni kubwa,

“Kwa ujumla, kasi ya usajili wa talaka ni kubwa na hii inaonyesha wazi kwamba migogoro katika ndoa inazidi kushika kasi. Juhudi za ziada zinatakiwa kwa wadau mbalimbali ili kupunguza tatizo hili,” alisema Hudson.

Taarifa za utafiti kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), zinaonyesha kuwa talaka nchini zimeongezeka kutoka asilimia 1.1 mwaka 2008/09 hadi asilimia 2.9 mwaka 2017/18 huku taarifa kutoka RITA zikibainisha kuwa kwa mwaka 2020/21 pekee, talaka 551 zilisajiliwa nchini.

Aidha, kwa Mkoa wa Dar es Salaam pekee, kwa mujibu wa Jaji Mkuu, Prof. Ibrahim Juma, katika hotuba yake jijini Dodoma, mashauri ya ndoa na talaka kwa mwaka 2017 hadi 2019 yalikuwa 4,200. 

“Inawezekana talaka ni nyingi kuliko takwimu hizi kwa kuwa watu wengi hawajui kusajili matamko ya talaka kutoka mahakamani ili wapate vyeti. Pia wako wanandoa ambao hutengana na kupeana talaka mitaani kienyeji pasipo kufuata taratibu za shEria,” alisema Mchungaji Dk. Enock Mlyuka, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Marriage and child Care (TaMCare) Foundation, asasi inayojishugulisha na masuala ya ndoa na malezi ya watoto.

Aliongeza kuwa takwimu hizo zinaonyesha kwamba migogoro na kuvunjika kwa ndoa ni janga la taifa, ndiyo maana taasisi yake imeamua kuanza kutafuta suluhisho la tatizo hilo.  

ATHARI KUBWA

Kutokana na kushamiri kwa migogoro na kuvunjika kwa ndoa, Dk. Mlyuka anabainisha kwamba kuekuwa na athari kubwa ambazo zinasababisha mmomonyoko wa maadili na kupungua kwa tija na ufanisi kazini.

“Migogoro na kuvunjika kwa ndoa kumesababisha kuongezeka kwa vitendo vya ukatili na unyanyasaji ndani ya ndoa na matokeo ya wanandoa na wapenzi kuuana. Waathirika wa vitendo hivi ni wanawake na watoto.

“Migogoro ya ndoa pia husababisha matatizo ya kiafya hasa msongo wa mawazo. Athari zake ni kubwa kiroho, kiuchumi, kisaikolojia na kiafya. Pia watoto wanaathirika zaidi katika makuzi yao na kukosa haki ya kuishi na wote wawili hivyo kusababisha mmomonyoko wa maadili,” alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA), Jaji Joacquine De Mello, aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa program hiyo, alisema ndoa ndiyo msingi wa kila kitu hivyo kliniki hiyo itasaidia kulipatia ufumbuzi tatizo hilo ambalo linatishia ustawi wa taifa.

“Tunaishi katika jamii inayobadilika kwa kasi. Kwa vyovyote vile mabadiliko haya hayaziachi ndoa na familia zetu salama. Tumeshuhudia uwapo wa mmomonyoko mkubwa wa maadili, hujuma na manyanyaso baina ya wanafamilia,” alisema.

Jaji De Mello alisema familia bora ni jambo muhimu kwa ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla, hivyo kupungua kwa migogoro ya ndoa kutawezesha kupungua kwa maradhi kama vile msongo wa mawazo na jamii kuishi katika amani na furaha.

“Maendeleo ya taifa yanahitaji ndoa imara. Ni ukweli usiopingika kwamba tukiwa na ndoa imara, tutakuwa na familia imara. Tukiwa na familia imara, tutakuwa na jamii imara na tukiwa na jamii imara, tutakuwa na taifa imara kwani ndoa ni msingi wa kila kitu,” alisisitiza. 

Chanzo: ippmedia.com