Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jinsi bodaboda 20 za Diamond zitakavyozalisha ajira Tandale

21227 DIAMOND+PIC TanzaniaWeb

Mon, 8 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Pikipiki 20 alizotoa mwanamuziki Nasib Abdul, maarufu Diamond kwa ajili ya vijana wa Tandale jijini Dar es Salaam zitatoa ajira kwa zaidi ya watu 50 kufikia mwakani.

Pikipiki hizo ambazo zilikabidhiwa kwa uongozi wa Kata ya Tandale juzi wakati akisherehea siku yake ya kuzaliwa, zitaingizwa kwenye biashara ya bodaboda na vijana watakaokabidhiwa, watatakiwa kuwasilisha Sh10,000 kila siku kwa muda wa miezi mitatu.

Meneja wa mwanamuziki huyo, Hamis Taletale maarufu Babu Tale alisema jana kuwa fedha zitakusanywa na kununulia pikipiki nyingine ambazo nazo zitasambazwa kwa vijana wengine.

Kwa hesabu ya Sh10,000 kwa siku pikipiki 20 zitakusanya Sh200,000 kwa siku sawa na Sh18 milioni kwa miezi mitatu kiasi ambacho kinatosha kununua nyingine tiisa zenye thamani ya Sh2 milioni kila moja.

Babu Tale alisema kama bodaboda hizo zitaendeshwa na kusimamiwa kwa umakini, zitawakwamua vijana wengi.

Aliongeza kuwa licha ya ukubwa wa tukio la msanii wake kutoa msaada wa bima, mitaji na pikipiki kwa wakazi wa Tandale, jambo hilo halikuwa kwenye mipango yao.

Alisema Diamond alifikiria kufanya hayo akiwa Namibia siku chache zilizopita na maandalizi yake yalifanyika ndani ya siku tatu.

Alisema kwa kuwa msanii wake siku zote amekuwa na ndoto ya kuacha alama kwenye jamii yake, walimuunga mkono na kuhakikisha hilo linatimia.

“Wiki iliyopita alienda Namibia, akiwa kule ndio akapata wazo la kufanya kitu cha tofauti kusherehekea siku yake ya kuzaliwa, akanipigia simu kunieleza tukakubaliana akirudi tujadili nini kifanyike aliporudi Jumanne tukaanza kupanga. Tukaona suala la kurudi Tandale kwa kuwawezesha vijana na wanawake kiuchumi ni wazo zuri na hata bima za afya ni msaada mkubwa, basi tukamshirikisha mlezi wetu (Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda)ambaye alisaidia kutuunganisha na uongozi wa Serikali wa Kata ya Tandale,” alisema Babu Tale.

Alifafanua kuwa fedha walizopewa wanawake 200 sio mkopo, bali mtaji wa kuwawezesha kufanya biashara ndogondogo katika maeneo hayo.

Kupitia mkusanyiko huo, pia Diamond alitangaza kumpatia gari mpiga picha wake aitwaye Lukamba kutokana na uchapakazi wake.

Lukamba alitumia ukurasa wake wa Instagram kuelezea hisia zake, “Hadi sasa nimekosa maneno ya kuandika yatakayoweza kubeba hisia zangu na furaha niliyonayo. Nimekuwa nikiandika na kufuta kila neno naona halijitoshelezi. Diamond amekuwa msaada sana kwa sisi vijana maskini. Mungu azidi kukupa moyo wa kidogo unachopata kugawana na wenzako.”

Watu mbalimbali walipongeza hatua hiyo ya Diamond kutumia sehemu ya mapato yake kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye uhitaji na kuwataka wasanii wengine kuiga mfano huo.

Mkongwe katika uandaaji matamasha nchini, Juma Mbizo alisema mafanikio anayopata msanii Diamond yanatokana na heshima aliyonayo.

“Siku zote amekuwa kijana mwenye heshima, unyenyekevu na kujali kazi ndiyo sababu leo amefika mahali alipo, vijana wengine waige mfano wake.

“Tatizo siku hizi vijana wakipata umarufu wanaanza kujiona tofauti na wana jamii yaani mtu ametoa wimbo mmoja anajiona staa,”

Jana muigizaji Steve Nyerere aliitisha mkutano wa waandishi wa habari kuelezea alivyoguswa na namna Diamond alivyosherekea siku yake ya kuzaliwa.

Steve alisema msanii huyo amefanya kitu kikubwa na ataacha alama kwenye jamii. “Huwa tunafanya sherehe zinazogharimu fedha nyingi kuadhimisha siku zetu za kuzaliwa huku tukisahau mafanikio tuliyonayo yanatokana na watu kuunga mkono sanaa zetu.

“Yaani Diamond hata kama alikuwa na dhambi 600 jana zote zimesamehewa kwa kile alichofanya, tunatakiwa wasanii kuiga mfano huu, kazi ya kusaidia jamii sio ya Serikali peke yake na mimi naahidi muda ukifika wa kusherehekea siku yangu ya kuzaliwa nitafanya kama yeye.”

Licha ya Babu Tale kueleza kuwa kutokuwapo kwa wasanii wengine katika shughuli hiyo ni kutokana na wao kutowaalika, Steve Nyerere alisema kutokuwepo kwao kunaleta taswira mbaya.

“Tumekuwa watu wa kubeza, ile shughuli ingekuwa Serena ungeona ambavyo wangejaa wakiwa wamevalia suti zao na magauni ya gharama, lakini kwa sababu ni kwenye jamii hali ndio kama ile,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz