Baada ya msanii wa kizazi kipya, Jay Melody kutamba na wimbo wake wa Nakupenda, amekiri umemuachia deni ya kufanya itakayohiti zaidi, kuhakikisha mashabiki wake wanaendelea kufurahia kazi yake.
Jay Melody amesema msanii anapata faraja anapoona kazi anayoifanya inapokelewa kwa ukubwa kwenye jamii kama ilivyo ya Nakupenda inayotamba kila kona.
"Wimbo wa Nakupenda ni mkubwa sana, hilo ni kama deni kwangu kuhakikisha kazi nyingine nitakazoziachia ziwe sehemu ya jamii kwa maana ya muziki unaowagusa;
"Ndio maana lazima msanii ajiweke karibu na jamii ili kuijua inataka kitu gani, hilo litafanya tuandae mashairi sahihi , kwa sababu hatujiimbii sisi wenyewe."
Amesema kazi ya muziki inahitaji umakini na utulivu, ili kuendana na matukio halisi yanayokuwepo kwenye jamii kila wakati, vinginevyo wengi wao wanaweza wakawa wanapishana na matukio.
"Mfano huo wimbo kuna watu waliopo kwenye mapenzi yaliyokolea, wakiusikia unawasaidia kuongeza uzito wa penzi lao, ndio maana unapigwa maeneo mbalimbali ya starehe kama harusi na matukio mengine yanayoendana na hayo," amesema.