Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jay Melody alivyosota miaka tisa ndani ya THT

49488 Pic+melody

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Jay Melody si jina geni masikioni kwani pamoja na umri mdogo wa miaka 28, amekuwa akifanya vitu vikubwa. Alijiunga na Nyumba ya Kukuza Vipaji (THT) mwaka 2008 akiwa hana wimbo wowote mpaka pale alipomwandikia Nandy wimbo wa ‘Kivuruge’ uliotoka 2017 na jina lake ndipo likaanza kukua.

Harakati za muziki, anasema, alizianza tangu 2006 huku akiwa anajishughulisha na kazi mbalimbali ikiwemo kutengeza masofa, kuuza mitumba na kupiga msasa milango - kazi ambazo anasema hazikuweza kumlipa kama alivyotarajia.

“Ni kutokana na mihangaiko yangu hii, ndipo nikapata wazo la kwenda kuomba kujiunga na THT kuangalia upande wa muziki labda unaweza kubadilisha maisha yangu,” anasema.

“Wakati nafika kulikuwa na wanafunzi kama 120 wanaofanyiwa usaili, lakini nashukuru baada ya mchujo watu 14 ndio walipita nikiwemo mimi.” Katika mchujo huo, anasema viongozi wa THT waliwaambia wale ambao hawakubahatika kupita wasingeweza kuwachukua wote na kuwaahidi huenda wakawaita katika darasa lingine baadaye iwapo nafasi itapatikana.

“Nakumbuka bosi Ruge (sasa marehemu) alisema hawezi kuwachukua wote na kuwataka wengine wakatafute njia nyingine za maisha na kuwaahidi kama itatokea nafasi ya darasa lingine atawaita,” anasema.

Pamoja na kukaa benchi kwa takribani miaka tisa bila kutoa wimbo, Jay anasema baada ya wimbo wa ‘Kivuruge’ kuachiwa na kufanya vizuri sokoni ndipo akaachia na wimbo wake ‘Goroka’.

Anasema kwa kipindi chote aliwekwa benchi huku akiambiwa anasubiriwa akue kisanii, kwani alikuwa bado na hofu ikizingatiwa kwamba alikutana pia na wasanii wakubwa.

Baada ya kuaminika, Jay Melody anasema alianza kupata michongo mbalimbali ukiwemo wa kumwandikia wimbo wa ‘Njiwa’ msanii Willy Paul wa Kenya akimshirikisha Nandy.

Kama vile haitoshi alimwandikia wimbo msanii Alicious aliyewahi kutesa na kibao cha ‘Posa ya Bolingo’.

Wakati kwa Nandy hakuishia kumwandikia tu Kivuruge, bali wimbo wa Bado uliopo kwenye albamu ya msanii huyo, pia ni kazi ya mikono yake na Aibu aliounogesha kwa kushirikiana na wasanii wengine kutoka THT akiwemo Ben Hauzimi.Mpaka sasa Jay Melody , ameshaachia vibao vinne ukiachilia mbali Goroka upo pia wa ‘Namwaga Mboga’, ‘Mikogo Sio’ na ‘Zeze’.

Atakachomisi kwa Ruge Mutahaba

Pamoja na kwamba kazi ya Mungu haina makosa, Jay Melody anasema watakosa vitu vingi kutoka kwa muasisi huyo wa THT. Moja ya mambo anayoyakumbuka ni namna alivyokuwa akiwaambia wasanii wengine wakubwa wanapopata shoo kuwabeba na wadogo wasiokuwa na majina, jambo ambalo mbali na kuwapatia kipato pia iliwawezesha kujulikana.



Chanzo: mwananchi.co.tz