Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jay Melody afunguka kuhusu kusaini Rekodi Lebo

JayMelody Sugar Video 600x320 Jay Melody.

Tue, 7 Nov 2023 Chanzo: JamboMail

Mwimbaji Jay Melody amesema anaweza kufanya kazi na lebo yoyote pale atakapoona kuna nafasi ya kukua zaidi kimuziki na kibiashara ila sio jambo la kukimbilia kwake kama anavyofanya muziki wake.

Utakumbuka asilimia kubwa ya wasanii Bongo wanaofanya vizuri na kupata namba kubwa za mauzo katika majukwaa ya kidigitali ya kusikiliza na kuuza muziki wapo chini ya rekodi lebo za wasanii wenzao au wadau lakini kwa Jay Melody mambo ni tofauti kabisa.

Anafanya vizuri na kupata namba kubwa hata kuwazidi wasanii waliyopo katika lebo kubwa, mathalani wimbo wake, Nakupenda (2022) umefikisha ‘streams’ milioni 75.8 Boomplay na ndio wimbo pekee wa Bongofleva uliosikilizwa zaidi katika jukwaa hilo.

“Tamaa yangu ni kufanya kazi na kufanikiwa, mimi ni mfanyabiashara naweza kufanya kazi na msanii yeyote na wa lebo yoyote ambayo itakuwa tayari au itakuwa biashara kwangu na mimi nitaona kitu kwao.” amesema.

“Mimi sio msanii wa kusema nianze kuwa na tamaa na lebo, mimi na tamaa na mafanikio, na tamaa ya kufanya kazi iende vizuri, kwa hiyo inapotokea mtu yeyote anataka ushirikiano na mimi kwenye kufanya kazi iendee inawezekana lakini sina tamaa ya kusema niende kwenye lebo yoyote.” amesema Jay Melody.

Utakumbuka Jay Melody amekulia kimuziki Tanzania House of Talent (THT) ambapo ndipo alipewa jina hilo na Ruge Mutahaba, anasema THT kwa sasa haihusiki na usimamizi wa muziki wake, walimfundisha muziki na tayari amehitimu kama wenzake.

“Nipo mwenyewe najitegemea, nafanya vitu vyangu, sipo ndani ya THT, pale ni kama Chuo kimenifundisha muziki, ni watu ambao bado tunashirikiana lakini sio kwamba nipo pale kama mwanafunzi.” amesema na kuongeza.

“Ukiwa pale bado wewe ni mwanafunzi wa THT, kama Barnaba huwezi kusema yupo THT, alikuwepo THT sasa hivi anafanya mambo yake.” amesema Jay Melody.

Ukiachana na Jay Melody, wasanii wengine waliowahi kupita THT ni Mwasiti, Barnaba, Linah, Amini, Ditto, Nandy, Jolie, Maunda Zorro, Benson, Ruby, Marioo, Vumi, Recho, Ibrah Nation, Mataluma, Makomando, Beka Ibrozama, Ally Nipishe n.k.

Chanzo: JamboMail