Hii inawahusu baadhi ya warembo ambao wakiitwa kwenye bata za wikiendi na wapenzi wao huwa wanakwenda na kijiji au kiringi cha marafiki zao!
Stori iko hivi; jamaa mmoja ameibua mjadala wenye hisia tofauti baada ya kuonekana kwenye video akikataa katakata kumnunulia chakula rafiki wa mpenzi wake aliyetinga naye kwenye mtoko wa wapenzi (date).
Inavyoonekana, jamaa alikuwa amemwalika mpenzi wake kwenye kiwanja ili wapate chakula cha pamoja na kubadilishana mawazo ila mpenzi wake akaja na rafiki yake.
Inaelezwa kuwa, jamaa huyo alisema chakula ambacho angemudu kununua kilikuwa chake na mpenzi wake tu na si vinginevyo.
Baadhi ya watu wanasema kuwa, jamaa huyo amemdhalilisha mpenzi wake na rafiki yake ambaye hakupewa chakula badala yake akawa amekaa pembeni akiwatazama wakila vinono.
Jamaa huyo na mpenzi wake wanaonekana kufurahia mlo wao bila kusumbuliwa na mtu mwingine kwenye meza yao huku mwanamke aliyejiongeza akionekana kusononeka.
Rafiki wa mpenzi wa jamaa huyo anaonekana akiwa ameketi huku mikono yake ikiwa mapajani mwake akitazama bila kutamka lolote.
Watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii wanaonekana kumrushia mate ya povu mpenzi wa jamaa huyo kwa kumruhusu rafiki yake kuaibishwa kwa njia hiyo huku wanaume wakimpongeza jamaa huyo kwa kumpunguza rafiki huyo wa mpenzi wake.
Wengi wanasema kisa hicho kina somo zuri kwa wengine ambao wakiitwa na wapenzi wao huita Bajaj na kujazana hadi kwenye siti ya dereva kwenda kudandia vyakula na vinywaji vya dezo, jambo ambalo ni tabia iliyo chafu ya warembo wengi wa Kibongo.