Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jakate: Msimpigie kura mshindi SZIFF kwa kuangalia umaarufu alio nao

33222 Pic+jokate Jokate Mwegelo, DC Kisarawe

Mon, 24 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mlezi wa Tuzo za filamu za Sinema Zetu International Film Festival(SZIFF), Jokate Mwegelo amewashauri watu kutowapigia kura washiriki kwa kuangalia umaarufu walio nao au mahaba walio nao kwao.

Tuzo zinazoandaliwa na kampuni ya Azam Tv, zilianza mwaka jana ambapo Gabo aliibuka mshindi bora wa kiume na mshindi wa jumla huku mrembo Wema Sepetu akiibuka mshindi kwa upande wa waigizaji wa kike.

Akizungumza leo Jumatatu, Desemba 24,2018 katika mkutano na waandishi wa habari, uliolenga kuelezea hatua ambayo mchakato wa tuzo hizo umefika, Jakate ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe amesema watu hawapaswi kuangalia umaarufu kama kweli wanataka kukuza sanaa hiyo na badala yake waangalie uwezo na kipaji cha mtu.

Amesema kwa kufanya hivyo kutasaidia pia kuja na vipaji vipya badala tasnia hiyo kutawaliwa na watu walewale kila siku na kupongeza hatua ya waandaaji ya kwenda hadi mikoani kusaka washiriki.

“Pamoja na  kwamba waandaaji wameamua kutoa nafasi kwa watengeza filamu kutoa majina ya wale wanaowaona ni bora katika kipengele cha mwigizaji bora wa kike na wa kiume, lakini hii katika upigaji kura haiwazuii kuchagua mnayemuona anafaa na nina imani hata hao waandaaji hawatatuletea mtu ambaye wanajua hastahili.”

“Kwani kwa kufanya hivyo hata wao watakuwa wanajinyima fursa ya kujitangaza na kazi zao, kwa kuwa kutoa mshindi nako kunaongeza kuaminiwa na jamii,” amesema.

Kwa upande wake, Meneja Miradi wa Azam Tv, Sofia Mgata amesema tangu wafungue pazia la kupeleka kazi hizo za filamu Oktoba 30, 2018,wameweza kukusanya kazi 235 mpaka ilipofika Novemba 30,2018 na kati ya hizo zipo filamu ndefu na fupi, tamthiliya makala na sinema.

“Timu yetu ya wataalam ilipita ikiwa inahusisha watu kutoka Cosota na Bodi ya filamu na wamefanikiwa kupita vituo nane katika mikoa mbalimbali nchini na kupata kazi zilizo bora,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa vipindi wa Azam, Yahaya Mohamed amesema filamu zote 140 zilizochaguliwa zitaanza kuonyesha katika chaneli ya sinema zetu kuanzia Januari 1 hadi 30,2019 ambapo watu wataweza kuangalia ni kazi gani wanaona ni bora na wasanii kabla ya kuelekea kuanza kupiga kura.

Wakati kwa upande wa sinema, amesema hizi zitaonyeshwa bure katika ukumbi wa sinema wa City Mall, ambapo majaji ndio watachagua zilizo bora.



Chanzo: mwananchi.co.tz