Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

JPM ALISIMAMIA MATIBABU YA BITCHUKA, KING KIKI

5fc2a0d96849750bf4c0f62e81ad6812 JPM ALISIMAMIA MATIBABU YA BITCHUKA, KING KIKI

Wed, 24 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

CHAMA cha Muziki wa Dansi Tanzania (Chamudata) kimesema kitamkumbuka, Rais John Magufuli kwa jinsi alivyohakikisha wasanii wanapata haki za kazi zao na kuwapatia bima za afya kwa gharama nafuu.

Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa Chamudata, Hassan Msumari alisema Rais Magufuli aliiagiza Ofisi ya Waziri Mkuu iwashughulikie wanamuziki wakongwe Hassan Rehani Bitchuka ‘Stereo’ na Kikumbi Mwanza Mpango, ‘King Kikii’ wawe wanatibiwa sehemu ya watu mashuhuri katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

“Kiukweli sisi wasanii tutamkumbuka kwa mengi, kwanza tumesaidiwa tumepewa bima ya afya kwa Sh 100,000 wakati watu wengine wanalipa tofauti na sisi, halafu Bitchuka anatibiwa kwa watu mashuhuri katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,” alisema Msumari.

Alisema Rais Magufuli alijibainisha kuwa ni mwenzao hata kwenye ziara za kitaifa alishindwa kuficha hisia zake na kwenda kuungana na wanamuziki na kupiga ngoma.

“Amepigania wasanii walionyonywa na kampuni walizofanya nazo kazi, mfano Mzee Majuto familia yake imekuja kupata haki ya baba yao baada ya mwenyewe kufariki na alihakikisha ofisi za Chama cha Hakimiliki Tanzania na haki shirikishi (Cosota) zinahamia Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo,” alisema.

“Kiukweli tumepoteza mtu mmoja makini sana, tumempoteza Rais wa wanyonge na shujaa wa Afrika nzima, nitamkumbuka kwa msimamo wake, lakini ndiyo hivyo, Mungu amempenda zaidi, tunamuombea apumzike kwa amani,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz