Wasanii wa filamu Jacob Steven maaarufu ‘JB’ na Salum Mchoma kwa jina la kisanii Chiki Mchoma wameteuliwa kuwa wajumbe wa bodi ya filamu Tanzania.
JB ni muigizaji na mtayarishaji filamu huku Chiki akiwa ni muigizaji, mwongozaji na Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji Tanzania.
Taarifa iliyotolewa leo na Mkuu wa Kitengo cha Mawasilino wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, John Mapepele, imesema uteuzi huo umefanywa na Waziri Mohamed Mchengerwa, kufuatia bodi ya awali kumaliza kipindi chake.
“Uteuzi huo umefanywa kwa kuzingatia mamlaka aliyopewa Waziri chini ya sehemu ya 13 ya sheria ya filamu na Michezo ya kuigiza namba 4 ya mwaka 1976 ambapo bodi hiyo inaundwa na Mwenyekiti na wajumbe sita na katibu Mtendaji ni Katibu wa bodi hiyo,” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha imemtaja Mwenyekiti wa bodi hiyo atakuwa ni Profesa Frowin Nyoni ambaye ni Mkurugenzi wa Uzamili Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na ameteuliwa kwa kipindi kingine cha pili.
Wakati wajumbe wa bodi na nafasi zao kwenye mabano ukiacha waigizaji JB na Chiki, yupo Keneth Kasigila (Mratibu wa Miradi Benki ya CRDB), Dk Mona Mwakalinga (Mhadhiri Mkuu, Idara ya Sanaa Bunifu, Chuo Kikuu cha Dar es Slamaam na Leah Kihimbi (Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Sanaa).
Aidha taarifa hiyo imesema kuwa uteuzi wa mjumbe mwingine anayewakilisha taaluma ya sheria utatangazwa baada ya taratibu husika kukamilika na uteuzi huo unadumu kwa miaka mitatu ambapo unaanzia Machi 25, 2022.