Kuna madai kuwa Jeshi la Polisi nchini linashikilia hati ya kusafiria ya mkali wa kibao cha 'Buga', Kizz Daniel baada ya kushindwa kufanya onyesho hapa nchini.
Mmoja wa watu anayejihusisha na masuala ya muziki katika kampuni ya Str8up music iliyomleta msanii huyo amedai kuwa baada ya kufanya majadiliano wakiwa polisi wamekubaliana hati hiyo ishikiliwe na wataendelea na mazungumzo nje ya Polisi.
Alipoulizwa kuhusika kwa Harmonize kumdhamini polisi msanii huyo, chanzo hicho kilisema jambo hilo halina ukweli wowote kwani msanii huyo alifika kumuona kama msanii mwenzake lakini hausiki na kumtoa.
Taarifa zaidi zinadai kuwa msanii huyo alishindwa kufanya show hiyo kwa kile kilichoelezwa kuwa kimetokana na kusahau begi lake lililokuwa na nguo na vito vya thamani jijini Nairobi nchini Kenya.
Licha ya kutafutiwa nguo na watu watatu tofauti akiwemo msanii Harmonize ili aweze kupanda jukwaani, aliweka kisingizio kingine cha kutokuwa na cheni.
Inadaiwa kuwa tabia ya msanii huyo, ilifanya kampuni hiyo iliyomleta kwenda kumshtaki polisi na zimeonekana video mbalimbali akiwa amefuatwa kwenye hoteli moja ya nyota tano iliyopo katikati ya jiji hilo na kupakizwa kwenye gari la polisi ambapo hata hivyo saa mbili usiku.
Mwanachi, limezungumza Kamanda wa Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam,Jumanne Muliro, ambaye amekiri suala hilo kutua mezani kwake na kueleza kuwa wanalishughulikia kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya sheria.
"Unajua hili suala lilivyokaa sio la kipolisi pekee, kuna mambo ya mikataba hivyo tunashirikiana na vyombo vingine vya kisheria.
"Tunafanya hivyo kila upande uweze kupata haki yake kwani ujio wake hapa kuna watu wamemleta na wamemlipa, kwa hiyo nadhani unavyoona lilivyokaa sio suala la kushughulikiwa na taasisi moja,"amesema Muliro.