Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

SIL

Ilikuwa ngumu familia kunielewa kuwa dereva

Derevaa15 Ilikuwa ngumu familia kunielewa kuwa dereva

Mon, 25 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

“Niliwaambia nimesomea upambaji, kushona lakini nimeiona hii ndiyo kazi ninayoweza kuifanya, hivyo niacheni ikifika mahali nimefeli nitaachana nayo kwa kuwa maisha ni kuchagua, jambo ambalo baadaye familia ilinielewa lakini jamii iliyonizunguka ilikuwa haielewi.”

Hata hivyo, Ihema ambaye pia ni dereva katika Kampuni ya Kuendesha Mabasi yaendayo Haraka (Udart) anasema hao hao waliokuwa wanamuona amepotea maisha, wanatamani kupanda gari analoendesha na wale anaobahatika kukutana nao barabarani hutaka kupiga naye picha.

Akitoa wito kwa wanawake, Ihema anasema wasiwe na wepesi wa kukata tamaa kwa kusikiliza maneno ya watu na kuonyesha jamii kuwa kazi zilizodhaniwa kuwa ni za wanaume, nao wanaweza kuzifanya vizuri zaidi.

Dereva huyo maarufu Madam Ihema anasema akiwa na wenzake kumi wameanzisha kikundi cha madereva wanawake kwa lengo la kusaidiana, lakini baadaye kukazalika wazo la kuanzisha Chama cha Madereva Wanawake Tanzania.

Anasema chama hicho kilianza mwaka 2020 kama kikundi cha wanawake, lakini kadiri siku zilivyoenda wakaona wapate wadau wengine na mpaka sasa chama kina zaidi ya wanachama 80 kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Dereva huyo anasema wingi wa idadi hiyo ya wanachama ilichagizwa zaidi madereva wanawake walipopata mafunzo Chuo cha Usafirishaji (NIT) kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia (WB).

Chama hicho ambacho kina madereva wa magari binafsi, ya Serikali, malori na magari ya shule malengo yake ni kusaidia kutoa elimu kwa wanawake kuwa udereva ni kama kazi nyingine.

"Tunashukuru tayari tumeshakisajili chama chetu mpaka sasa na kinachosubiriwa ni kufanyika uzinduzi tunaotarajia hadi ifikapo Machi mwakani tuwe tumefanya hivyo,"anasema Madam Ihema.  

Majukumu ya chama

Akieleza majukumu ambayo chama kitakuwa kikiyafanya, Ihema ambaye ni mama wa mtoto mmoja anasema ni kutoa elimu kuhusu chama hicho.

"Kwa kutoa elimu kuhusu chama, jamii itaelewa kuwa madereva wanawake wapo wengi tu na sio mmoja mmoja kama wanavyomuona huko barabarani wakiwa wanaendesha vyombo mbalimbali vya moto,"anasema Madam Ihema.

Majukumu mengine anasema ni kutetea haki zao na kuendelea kupokea wanachama.

Pia, anasema kupitia chama hicho wataweza pia kuhamasishana kwenda kuongeza kiwango chao cha elimu.

"Ili uwe dereva wa magari makubwa itakupasa kuwa na daraja C na hii ni kwa kuwa chama chetu kinachukua dereva wa aina zote, akiwamo wa gari binafsi, magari ya biashara, wasio na kazi kokote lakini wanaweza kuendesha gari," anasema Madam Ihema.  

Matarajio

Malengo yao anasema ni kuanzisha mradi wa magari ya kukodisha kama coaster na mabasi ya kwenda mikoani na kwamba madereva wake na utingo watakuwa wanawake pekee.

Lengo lingine anasema ni kuwa na chuo cha madereva wanawake kama ilivyo kwa shule za watoto wa kike pekee.

"Tunataka kufanya hivi ili wanawake wawe huru zaidi kusomea udereva kwa kuwa kuna ambao hawapendi kujichanganya na wanaume; kwa kufanya hivyo itawapa uhuru zaidi wanawake hao madereva kusoma,” anasema Madam Ihema.  

Vipi kuhusu changamoto?

Akielezea kuhusu changamoto wanazozipata madereva wanawake, Madam Ihema anasema ni katika upatikanaji wa kazi tofauti na wanaume.

Anasema ili mwanamke apate kazi ni mpaka aonekane anaendesha chombo barabarani ndio anaaminika kweli ni dereva.

"Utakuta mtu amekuona unafanya kazi mahali ndio anakuambia naomba uhame hapo uje kwetu, lakini unapokwenda na vyeti vyako kuomba kazi wengi huwa wakipuuza na kuona hawezi," anasema Madam Ihema.  

Alianzaje kazi ya udereva?

Madam Ihema anasema kazi ya udereva aliianza mwaka 2014 alipoagiza gari lake kutoka Japan.

Anasema wakati anaagiza gari hilo alikuwa hajui kuendesha, hivyo alikwenda Chuo cha Ufundi (Veta) kusomea udereva.

“Nikaenda Veta kuomba kusoma, nikapata nafasi, nikaingia darasani na nikasoma pale mwezi mmoja nikamaliza, lakini mwisho wa siku nikajikuta nanogewa na fani ya udereva,” anasema Madam Ihema.

Akiwa huko akapata wazo la kujiongeza kusoma na ndipo aliposomea kuendesha gari la kubeba mizigo mizito.

Baada ya hapo akapata kazi kiwanda cha bia na aliendesha gari hilo kwa muda wa mwaka mmoja kabla hajapata mafunzo ya udereva yaliyodhaminiwa na WB. Katika mafunzo hayo anasema kulikuwa na hatua za kusoma, hatua ya kwanza alisoma na kufaulu akaingia hatua ya pili ya kusomea kuendesha mabasi ya mikoani akafaulu na hatua ya tatu akasomea kuendesha mabasi ya mwendo wa haraka.

Mafunzo hayo alisoma mwaka mmoja kuanzia 2019 hadi 2020. Anasema ilipofika mwaka 2021 alipata kazi Udart anayoifanya hadi sasa.  

Alikuwa na shughuli gani kabla

Kabla ya kuingia katika masuala ya udereva, anasema alikuwa anafanya shughuli zake za ujasiriamali.

Anasema alikuwa akisimamia shule yake ya chekechea, lakini pia ni mshereheshaji, kazi anayoifanya pia hadi leo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live